Uturuki yajiandaa kuingia Syria na madhara yake Magazetini
8 Oktoba 2019Tunaanzia Mashariki ya kati ambako Marekani imewaondowa wanajeshi wake kaskazini mashariki mwa Syria na kuwafungulia mlango kwa njia moja au nyengine wanajeshi wa Uturuki kuingia nchini humo. Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linatathmini hatari inayoweza kutokea pindi Uturuki ikiingilia kati nchini Syria na kuandika: "Uvamizi wa Uturuki unaweza, hata kama si moja kwa moja, kuwapa nguvu tena wafuasi wa itikadi kali wanaojiita wa dola la kiislam-IS. Wanajeshi wa kikurd, ambao tangu IS waliposhindwa msimu wa kiangazi uliopita wamekuwa wakiwatia kishindo IS kwa ushirikiano pamoja na wanajeshi wa Marekani, mashariki mwa Syria, huenda wakalazimika kuzihama kambi zao ili waweze kukabiliana na wanajeshi wa Uturuki.
Wanamgambo wa IS wanaojiandaa tangu miezi kadhaa sasa kuanza mashambulio wanaweza kwa namna hiyo kuyateka upya maeneo ya Syria na kuwavutia tena wafuasi wa itikadi kali kutoka Ulaya. Mizani ya nguvu katika nchi iliyogubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ya Syria itabadilika, hali itakayopelekea vita kurefushwa na mikururo ya watu kuyahama upya maskani yao. Ulaya isitegemee kwamba itanusurika na hali mpya itakayozuka."
Wasyria wamechoshwa na vita
Gazeti la Badische Zeitung linasema kitu cha mwisho wanachokihitaji wa-Syria wakati huu tulio nao si vita. Gazeti linaendelea kuandika: "Katika maeneo mengi yaliyokombolewa, uharibifu ni mkubwa kwa namna ambayo maisha hayawezekani. Vita vinatishia kuripuka, na inaonyesha rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameshaamua vikosi vya nchi yake viiingie kaskazini mwa Syria, licha ya onyo la Umoja wa ulaya. Watakaoteseka zaidi na hali hiyo ni raia wa wanaoishi kaskazini mwa Syria."
Vuguvugu la wanaopigania usafi wa mazingira linawekewa suala la kuuliza
Vuguvugu la wanaharakati wanaopigania usafi wa mazingira wanaojiita "Extinction Rebellion" wameanzisha maandamano ili kuzishinikiza sereikali za dunia zipitishe hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kinyume na vuguvugu la vijana "Fridays for Future, vuguvugu hili jipya linawataka wanaharakati wake wasitii amri za serikali. Gazeti la Weser-Kurier linaukosoa msimamo huo na kuandika: "Haisaidii kitu hata kama wanasisitiza kama maandamano yao yatapita salama. Kwa kuzifunga njia na hatua nyenginezo za aina hiiyo inadhihirika tu kwamba kundi dogo linataka kuwalazimisha walio wengi wafuate msimamo wao-na hilo haliwezekani hata kidogo katika nchi inayofuata sheria."
Mandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Sekione Kitojo