Uturuki yasema haina nia ya kuchukua eneo lolote la Syria
10 Januari 2025Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, wakati akizungumza na waandishi habari mjini Istanbul.
Wasiwasi umekuwa ukiongezeka kuhusu kitisho cha Uturuki dhidi ya vikosi vya Kikurdi katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita.
Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema umoja huo unaweza kupunguza hatua kwa hatua vikwazo vya Syria ikiwa maendeleo yataonekana.
Soma pia: Mapigano Kaskazini Mashariki mwa Syria yasababisha vifo vya watu 23
Kallas amesema vikwazo hivyo vinaweza kuondolewa iwapo viongozi wapya watachukua hatua za kuunda serikali yenye kuyashirikisha makundi yote na inayowalinda watu wachache.
Matamshi hayo ameyatoa leo mjini Brussels, siku moja baada ya mkutano wa mataifa yenye nguvu ya Magharibi uliofanyika mjini Rome.