1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUturuki

Uturuki yashambulia ngome za Wakurdi nchini Syria na Iraq

26 Desemba 2023

Uturuki imetanua kampeni yake ya kijeshi dhidi ya makundi ya Wakurdi huko Syria na Kaskazini mwa Iraq ikiwa ni jibu kwa vifo vya wanajeshi wake 12 vilivyotokea nchini Iraq mwishoni mwa juma lililopita.

Ndege ya jeshi la Uturuki
Uturuki imekuwa ikitumia mashambulizi ya anga kwenye kampeni yake dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi.Picha: Eren Bozkurt/AA/picture alliance

Ndege za kivita za Uturuki zimeyalenga maeneo inayosema kuwa ni ngome za makundi ya Kikurdi na kusababisha vifo vya raia wanane nchini Syria ikiwemo wanawake wawili. Idadi hiyo ya vifo imetolewa kupitia mtandao wa X na msemaji wa vikosi vya wapiganaji wa Syria vinavyoongozwa na Wakurdi, Farhad Shami.

Kwa upande wake wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema imewauwa wanamgambo 26 wa Kikurdi kwenye mashambulizi yake iliyofanya kwa kutumia ndege za kivita.

Uturuki ilianzisha oparesheni hiyo baada ya  askari wake 12 kuuwawa kwenye mashambulizi mawili tofauti kaskazini mwa Iraq ambayo serikali mjini Ankara inasema yaliyofanywa na makundi ya wapiganaji wa Kikurdi.