Uturuki yasisitiza kupinga Sweden na Finland kujiunga NATO
19 Mei 2022Kiongozi huyo wa Uturuki ametoa msimamo huo kwa mara nyingine leo wakati akizungumza na shirika la utangazaji la Uturuki TRT na kusema msimamo wa serikali ya Ankara haujabadilika.
Amearifu kwamba tayari serikali yake imewaeleza viongozi wa NATO juu ya nia ya Uturuki ya kukataa maombi ya Finland na Sweden kujiunga na muungano huo wa kijeshi.
Mataifa hayo mawili ya Scandinavia yaliomba kujiunga na NATO mapema wiki hii katika mabadiliko makubwa ya sera ya ulinzi ya kutofungamana na upande wowote kijeshi iliyokuwepo kwa miongo mingi. Yote hayo yametokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambao umezidisha hamkani mjni Stockholm na Helsinki.
Hata hivyo baada ya maombi yao kupokelewa mara moja Uturuki ilizuia kuanza kwa majadiliano ya kuzikaribisha nchi hizo mbili yaliyopangwa kuongozwa na baraza kuu la NATO.
Uturuki inazituhumu Sweden na Finland kuwaunga mkono Wakurdi
Uturuki inasema Sweden na Finland zinakiunga mkono chama cha siasa cha wakurdi cha PKK kilichopigwa marufuku nchini Uturuki chini ya madai ya kufadhili ugaidi.
Kadhalika inazituhumu nchi hizo mbili kuliunga mkono tawi la wapiganaji wa Kikurdi la YPG linaloendesha shughuli zake kutokea Syria.
Msimamo uliotangazwa leo na Erdogan umesisitizwa pia na waziri wake wa mambo ya kigeni Mevlut Cavusoglu aliye ziarani nchini Marekani. Kwenye mkutano na mwenzake wa Marekani Antony Blinken, Cavusoglu amesema Uturuki haibadili msimamo hadi ipatiwe majibu juu ya namna mashaka inayoyaeleza kuhusu Finland na Sweden yatakavyoshughulikiwa.
"Tunaelewa wasiwasi wa usalama wa Finland na Sweden lakini wasiwasi wa usalama wa Uturuki nao ni sharti utatuliwe na hili ni jambo ambalo ni lazima tuendelee kulijadili na marafiki na washirika ikiwemo Marekani" amesema Cavusoglu.
Marekani ´yajitutumua´ kufanikisha uachama wa Sweden na Finland
Kwa upande wake Marekani inaonesha bado inatafuta uhakika juu ya uthabiti wa msimamo wa Erdogan licha ya kujaribu kuonesha kuyapuuza matamshi ya kiongozi huyo Erdogan mbele ya macho ya umma.
Waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken amesijinasibu kuwa Washington itahakikisha mchakato wa kuongeza wanachama wa NATO unafanikiwa. Japo hajasema ni vipi hilo litawezekana.
Kwa sababu chini ya kanuni za NATO wanachama wote 30 inafaa waridhie kukaribishwa mwanachama mpya. Na kila taifa lina kura ya turufu inayoweza kutumika kuzuia ombi la nchi mpya kujiunga na jumuiya hiyo.
Jioni hii rais wa Marekani Joe Biden amewakaribisha ikulu waziri mkuu wa Sweden Magdalena Andersson na rais wa Finland Sauli Niinisto kwa mazungumzo ya kina kuhusu NATO.
Ni dhahiri msimamo wa Uturuki utakuwa ajenda ya kipaumbele huko White House. Na wote wataumiza vichwa kutafuta majibu ya kutuliza munkari wa mjini Ankara.