1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatakiwa iheshimu masharti

1 Agosti 2016

Umoja wa Ulaya umesema Uturuki lazima iheshimu masharti yote ya makubaliano ya wahamiaji yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili, kabla ya kupewa hadhi ya raia wake kusafiri Ulaya bila ya kutumia visa.

Picha: Getty Images

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Mina Andreeva amesema leo kwamba kama Uturuki inataka wananchi wake wasafiri Ulaya bila ya kutumia visa, lazima itimize vigezo walivyowekewa. Andreeva amesema suala la visa ni sehemu ya vipengele vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya kwa Uturuki kuwazuia wahamiaji kuingia Ulaya na kuwachukua tena maelfu wengine zaidi.

''Halmashauri ya Umoja wa Ulaya bado ina nia thabiti ya kuhakikisha inaendelea na utekelezaji kamili wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya umoja huo na Uturuki. Pia tunatarajia washirika wetu Uturuki, watafanya vivyo hivyo. Kwa upande wetu, halmashauri imeendelea kuheshimu na hata kuharakisha utekelezaji wa ahadi zetu kulingana na mkataba wa miezi iliyopita kwa kuchukua hatua maalum wiki iliyopita,'' alisema Andreeva.

Umoja wa Ulaya umeanisha kuwa Uturuki bado inatakiwa kutimiza masharti matano ili kuhakikisha inajipatia hadhi hiyo, ikiwemo kubadilisha namna inavyoutafsiri ugaidi, ili waandishi wa habari na wana taaluma wasiwe walengwa.

Rais Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/U. Bektas

Hapo jana, wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilisema itajiondoa katika makubaliano hayo, iwapo hakuna tarehe itakayowekwa karibuni na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kutimiza ahadi ya kuwaruhusu raia wa Uturuki kuingia kwenye nchi za Ulaya bila visa.

Uturuki yaikosoa Ujerumani

Ama kwa upande mwingine, Uturuki imeukosoa uamuzi wa mahakama ya Ujerumani ambao umemzuwia Rais Recep Tayyip Erdogan kuwahutubia watu waliokuwa wakiandamana Ujerumani, wakilaani jaribio la mapinduzi la Julai 15.

Mahakama hiyo ilipiga marufuku kuonyesha ujumbe wowote wa wanasiasa nchini Uturuki kupitia njia ya video, katika maandamano hayo yaliyofanyika kwenye mji wa Cologne, na kuhudhuriwa na kiasi ya watu 40,000 kupinga jaribio la mapinduzi na kumuunga mkono Rais Erdogan.

Aidha, Uturuki imemuita balozi wa Ujerumani nchini humo kwa lengo la kutoa malalamiko yake kutokana na kitendo hicho. Balozi huyo alikuwa anatarajiwa kufika katika wizara ya mambo ya nje ya Uturuki leo, kulizungumzia suala hilo, wakati ambapo uhusiano baina ya nchi hizo mbili na nchi washirika ukizidi kudhoofika.

Maandamano ya wafuasi wa Erdogan, ColognePicha: Reuters/T. Schmuelgen

Kwa upande wake Ujerumani imesema inapitia katika kipindi kigumu cha uhusiano wake na Uturuki, lakini uzoefu wa nyuma unaonyesha kuwa suala hilo linatatulika, kwani nchi hizo mbili zina uhusiano wa karibu.

Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim leo anatarajiwa kukutana na mkuu wa jeshi la Marekani, Jenerali Joseph Dunford, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa aina yake tangu liliposhindikana jaribio la mapinduzi na kusababisha kukamatwa kwa maelfu ya watu, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu katika vikosi vya kivita vya Uturuki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP,DPA,RTR
Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi