1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatakiwa kuchukua hatua dhidi ya IS

Elizabeth Shoo21 Oktoba 2014

Habari moja inayozungumziwa magazetini ni mapambano kati ya Dola la Kiislamu na wapiganaji wa Kikurdi katika mji wa Kobane. Wahariri wamegusia pia mjadala wa kiuchumi kati ya ujerumani na Ufaransa.

Mji wa Kobane bado unapiganiwa
Picha: picture-alliance/AP Photo/Lefteris Pitarakis

Mhariri wa gazeti la "Berliner Zeitung" anaikosoa serikali ya Uturuki akisema: "Rais Erdogan na waziri mkuu Davutolu hawafanyi lolote kuwasaidia wakurdi wanaoutetea mji wa Kobane. Wako radhi mapigano yaongezeke kuliko watumie nguvu dhidi ya kundi la IS. Lakini kundi hilo kwa sasa linatawala kilometa mia tatu za mpaka kati ya Uturuki na Syria."

Gazeti la "Mannheimer Morgen" pia linamnyooshea kidole rais Erdogan na kusema kwamba kiongozi huyo ana bahati kuwa waasi wa IS bado hawajafanikiwa kuuteka mji wa Kobani. Mhariri wa gazeti hilo anaandika: Erdogan amefanya makosa mengi katika kuyakabili makundi ya IS na PKK. Amesahau kwamba wakurdi wanaweza kulipiza kisasi kwasababu yeye amekataa kuwasaidia. Labda shinikizo kutoka Marekani sasa limemfanya rais huyo apige hatua ya kwanza.

Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linazungumzia watu wanaotoka Ujerumani na kwenda kujiunga na mapigano ya Dola la Kiislamu huko Iraq na Syria. Mhariri wa gazeti hilo anasema: Ni hatua ya muhimu kwa waziri wa sheria wa Ujerumani kutangaza kuwa wapiganaji hao watazuiwa kusafiri nje ya nchi. Lakini haieleweki kwanini waziri huyo hataki kuwabana kisheria wale ambao tayari wameingia vitani. Watu hao ni kama mabomu yanayosubiri kulipuka. Kama wana uraia wa nchi mbili basi wanyang'anywe uraia wa Ujerumani.

Ufaransa yataka Ujerumani iwekeze zaidi

Waziri wa uchumi wa Ufaransa Emmanuel Macron alikutana na waziri wa fedha wa Ujerumani kuzungumzia mikakati ya kukuza uchumi. Macron alisema Ufaransa itabana matumizi kwa kiasi cha Euro billioni 50 iwapo Ujerumani itawekeza kiasi hicho hicho cha fedha. Kuhusu tamko hilo mhariri wa "Thüringische Landeszeitung" anasema: Tangu rais Francois Hollande achukue madaraka, uchumi wa Ufaransa umeporomoka kwa kasi. Serikali ya nchi hiyo imegoma kuleta mageuzi ya sera, badala yake inaendelea kuongeza madeni.

Waziri wa uchumi wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Reuters/J. Naegelen

Hivyo inashangaza kuona kwamba waziri Emmanuel Macron anadiriki kuishinikiza Ujerumani kurudia makosa kama ya Ufaransa. Hata kama Ujerumani itawekeza Euro Billioni 50, haitasaidia kuuboresha uchumi wa Ufaransa.

Naye mhariri wa "Kieler Nachrichten" anasema wachumi wa hapa Ujerumani wanakubaliana kwamba serikali lazima iwekeze zaidi katika miundombinu ili kuliimarisha sokola ndani la Umoja wa Ulaya. Mhariri huyo anaamini kwamba hatua hiyo huenda ikaisaidia Ufaransa kupambana na matatizo yake ya uchumi. Lakini anaonya kwamba hiyo si njia ya kuyamaliza kabisa matatizo hayo kwani serikali ya Ufaransa kwa miaka mingi imekuwa na matumizi makubwa kuliko mapato. Hata kama Ujerumani itasaidia, serikali ya Hollande haitaepuka kupunguza matumizi yake kwa kiasi kikubwa.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW