Uturuki yatuma majeshi Syria
13 Oktoba 2017Uturuki ilisema operesheni yake eneo hilo ni mojawapo ya maazimio yaliyoafikiwa mwezi Septemba pamoja na Urusi na Iran huko Astana, Kazakhstan ili kupunguza mapigano baina ya wanamgambo na serikali ya Syria.
Gazeti la Uturuki la Hurriyet limesema zaidi ya wanajeshi 100 kikiwemo kikosi maalum na magari 30 ya kivita yaliingia Idlib na likaripoti kuwa huenda wanajeshi zaidi wakatumwa katika eneo hilo katika siku chache zijazo.
Jeshi la Uturuki linaunga mkono waasi wa Syria wanoiunga mkono serikali ambao wanataka kuwaondoa wanachama wa Hayat Tahrir al-Sham katika eneo hilo ili kutoa nafasi kwa vikosi vya Iran, Urusi na Uturuki katika eneo hilo katika harakati za kupunguza mapigano.
Mashirika ya haki za kibinadam yanasema hatua hiyo ni ya kutoa ujumbe
Hatua hii inajiri baada ya jeshi la Uturuki kuanza kuchunguza eneo hilo Jumapili kama mojawapo ya harakati za Uturuki pamoja na Urusi na Iran kuzingatia yale yaliyoafikiwa katika yale mazungumzo ya amani ya Astana yaliyo na lengo la kufikisha kikomo mzozo wa Syria.
"Kwa kufanya matayarisho tunalenga kutambua maeneo ambayo tutawatuma wanajeshi," alisema Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildrim. "Wanajeshi wa Uturuki watafanya majukumu yao kulingana na makubaliano kati ya nchi zilizokuwa Astana," aliongeza Waziri huyo Mkuu.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu lililo na makao yake Uingereza Syrian Observatory for Human Rights lilisema hatua hiyo ya kutuma wanajeshi inalenga kutoa ujumbe wa uwepo wa wanajeshi wa Uturuki katika eneo la mpaka wa mkoa wa Idlib na eneo la Wakurdi, jambo lililothibitishwa na mpiganaji mmoja wa waasi katika eneo hilo.
Mwanamgambo mmoja wa Kikurdi alisema wanajeshi waliowasili katika eneo hilo sio wengi kwa sasa.
Uturuki imekuwa ikiwaunga mkono waasi wanaompinga Bashar al-Assad
Waziri mkuu Yildrim alielezea uamuzi wa Uturuki kuchukua hatua hiyo kama utakaozuia matukio ya kigaidi katika eneo hilo.
"Chini ya uamuzi huu, Idlib itawekwa chini ya ulinzi na nchi tatu zilizohusika katika yale mazungumzo ya Astana na kutokana na hilo Matukio ya kigaidi yatazuiwa," alisema Yildrim. "Kwa upande mwengine tutazuia uhamiaji mkubwa wa wakimbizi wanaokimbia machafuko ya nchini Syria kuingia nchini mwetu," aliongeza Waziri huyo Mkuu.
Uturuki siku zote imekuwa shabiki mkubwa wa waasi wanaopigana dhidi ya rais wa Syria Bashar al-Assad lakini tangu mwaka jana, nchi hiyo imejikita katika kuuweka salama mpaka wake ili usishambuliwe na Wakurdi wanaodhibiti sehemu kubwa ya Syria na magaidi.
Mzozo wa Syria ulianza baada ya maandamano makubwa dhidi ya serikali mwaka 2011, lakini tangu wakati huo mzozo huo umegeuka vita vikubwa ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 330,000.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman