Uturuki yaukosoa uamuzi mpya wa Marekani juu ya Jerusalem
24 Februari 2018Tangazo hilo la Ijumaa (23 Februari) la Marekani la kuuhamisha ubalozi huo kutoka Tel Aviv kuelekea kwenye mji wenye utata unafuatia uamuzi wa Rais Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel mnamo Disemba 2017.
Kwa mujibu wa Uturuki, uamuzi huu ulionesha namna Marekani isivyosikiliza na "kibaya zaidi, isivyojali sauti ya jamii ya kimataifa" kwenye suala la Mashariki ya Kati.
"Uamuzi huu unaonesha dhamira ya Marekani katika kuiharibu misingi ya amani kwa kuvunja sheria za kimataifa, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya Jerusalem," ilisema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, ikiongeza kwamba nchi hiyo "itaendelea na jitihada zake za kulinda haki za kisheria za umma wa Wapalestina...dhidi ya uamuzi huu unaogofya sana wa Marekani."
Israel yafurahikia tangazo la Trump
Lakini wakati Uturuki ikililaani tangazo hilo la Marekani, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alilipongeza akisema kuwa siku hiyo itakuwa tukufu sana kwa watu wa Israel.
"Uamuzi wa Rais Trump kuuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerusalem katika Siku ya Uhuru inafuatia tangazo lake la kihistoria la mwezi Disemba kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel," ilisema taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Israel nchini Marekani siku ya Ijumaa.
"Uamuzi huu utaigeuza siku ya Maadhimisho ya 70 ya Uhuru kuwa kubwa zaidi. Ahsante Rais Trump kwa uongozi na urafiki wako," iliongeza taarifa hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kiabrenia.
Palestina yalaani vikali
Tangazo hili la Marekani lilipokelewa kwa hasira kali na upande wa Palestina. Kiongozi wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Saeb Erakat, aliukosoa muda uliopangwa kutolewa kwa tamko hilo, akisema inaonesha "dhamira ya utawala wa Marekani ni kuzichafua sheria za kimataifa, kuharibu suluhisho la madola mawili huru, na kuchochea hasira za watu wa Palestina."
Wapalestina hukumbuka kile wanachokiita Nakba, yaani wimbi kubwa la Wapalestina kuhama nchi yao kufutia kuanzishwa kwa taifa la Israel, siku ya tarehe 15 Mei, huku Marekani ikisema inapanga kuuhamishia ubalozi wake siku ya kuanzishwa kwa dola hilo, tarehe 14 Mei.
Wakati wa vita vya Waarabu na Waisrael vya mwaka 1948, ambavyo vilifuatia kuundwa kwa Israel, takribani Wapalestina 700,000 walikimbia makaazi yao na hivyo kuanza kuwa wakimbizi hadi leo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Isaac Gamba