1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yavutana na Marekani kisa Padri

1 Agosti 2018

Washirika wawili wa NATO wameingia kenye mvutano wa kidiplomasia kuhusiana na kifungo cha nyumbani dhidi ya padri wa Kimarekani anayeishi na kufanya kazi Uturuki.

Symbolbild USA Türkei Beziehungen (Ausschnitt)
Picha: Imago/imagebroker

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema lugha ya vitisho inayotumiwa na Marekani haitomfaidisha mtu yoyote.Kauli hiyo ya Erdogan imekuja katika wakati ambapo uhusiano kati ya washirika hao wawili wa jumuiya ya kujihami ya NATO umezidi kuvurugika kuhusiana na kisa cha kufungwa kwa padiri wa kimarekani katika jela ya Uturuki akituhimiwa kuhusika na ugaidi.

Akizungumza na waandishi habari mjini Ankara rais huyo wa Uturuki amesema nchi yake haitopiga magoti kufikia mwafaka wa aina yoyoyte linapokuja suala la uhuru wa vyombo vyake vya sheria na kuongeza kwamba mtazamo wa Marekani wa kiinjilisti na kizayuni haukubaliki. Erdogan amebaini kwamba waziri wake wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu atafanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Michael Pompeo pembeni kwa mkutano wa jumuiya ya nchi za Asia ASEAN utakaofanyika Singapore.

Padri Andrew Brunson aliyekuwa akiliongoza kanisa la kiprotestanti katika mji wa Izmir aliwekwa katika kifungo cha nyumbani wiki iliyopita baada ya kiasi miaka miwili ya kukaa jela.Hata hivyo mgogoro huo umekuwa ukizidi makali ambapo hivi sasa maafisa wa Marekani wameghadhabishwa na hatua ya padiri huyo kutoruhusiwa kuondoka nchini Uturuki.Rais Donald Trump na makamu wake Mike Pence wameitishia Uturuki na vikwazo vikali ikiwa padiri huyo hatoachiwa huru.

Padri Andrew BrunsonPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/E. Tazegul

Na hicho ndicho haswa leo kilichomvuruga rais wa Uturuki aliyeibuka na kusema kwamba katu nchi yake haiwezi kuitilia maanani lugha hiyo ya vitisho ya Marekani.Makamu wa rais wa Marekani Pence alisema wiki iliyopita kwamba Brunson ni mhanga wa mateso  kutokana na imani yake ya kidini  ingawa kwa upande wake rais wa Uturuki anasisitiza kwamba nchi yake haijawahi hata siku moja kuwa na tatizo dhidi ya watu wachache wenye dini tafauti.Matamshi ya Erdogan yanakuja baada ya viongozi wa ngazi ya juu kutoka dini za waliowachache nchini Uturuki kutoka taarifa ya pamoja leo wakikanusha kwamba kumekuwa na shinikizo dhidi ya wafuasi wao.

Brunson anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 35 jela ikiwa atakutwa na makosa ya kuhusika na tuhuma za kuyasaidia makundi mawili yanayotajwa na Uturuki kuwa ya kigaidi,kundi la harakati linaloongozwa na ulamaa wa kiislamu aliyeko Marekani Fethulla Gulen na kundi la wafanyakazi wakikurdi PKK. Kadhalika padiri Brunson anatuhumiwa kutumiwa kufanya udukuzi wa kisiasa na kijeshi,ingawa anazikanusha tuhuma zote hizo na maafisa wa Marekani pia wanamkingia kifua wakisema hana hatia.

Jana mahakama ilikataa ombi lililowasilishwa na wakili wa Brunson la kutaka mteja wake aachiwe huru.Wakati mvutano wa kidiplomasia ukizidi kuongezeka kati ya Marekani na Uturuki  Kesi hiyo imepangwa  itasikilizwa tena Oktoba 12.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFP/ARTE

Mhariri:Josephat Charo