1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Uturuki yawakamata watu 110 kwa madai ya kigaidi

25 Aprili 2023

Polisi ya Uturuki imewakamata watu 110 kwa madai yanayofungamana na kundi la kigaidi.

Türkei Ankara Polizeieinsatz
Picha: Tunahan Turhan/Zuma/IMAGO

Mbunge mmoja anayegemea upande wa Wakurdi amesema wanasiasa, mawakili na waandishi habari ni miongoni mwa wale wanashikiliwa na polisi baada ya msako huo ambao umejiri kuelekea uchaguzi mkuu wa Mei 14. 

Msako huo wa polisi ulifanywa hasa Diyarbakir ambao ni mji mkubwa zaidi na ambao wakaazi wake wengi ni Wakurdi upande wa kusini mashariki mwa Uturuki.

Misako ilifanywa pia katika mikoa 21 huku maafisa wa polisi wakiwalenga watu waliodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la wanamgambo la chama cha wafanyakazi cha Wakurdi ambacho kimepigwa marufuku (PKK).

Msako huo umejiri wiki tatu tu kabla ya uchaguzi mkuu wa urais na ubunge kufanyika nchini humo.

Uchaguzi mkuu Mei 14

Uchaguzi huo unatizamwa kuwa mtihani mkubwa kwa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan tangu chama chake cha AK kilipochukua madaraka mwaka 2002.

Soma pia: Mpinzani mkuu wa Erdogan anawatetea Wakurdi

Mbunge wa chama cha People's Democratic Party (HDP) Tayip Temei, amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba kutokana na hofu ya kushindwa kwenye uchaguzi, serikali imeamua kutumia mbinu ya kuwakamata watu tena.

Amesema makumi ya wanasiasa, wakiwemo wakuu wa chama chake, waandishi wa habari, wasanii na mawakili, ni miongoni mwa wale waliotiwa mbaroni mjini Diyarbakir.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mjini Diyarbakir ilikataa kutoa kauli kuhusu msako huo.

Duru ya habari ya kiusalama imesema polisi walifanya msako kwenye majumba 186 na kwamba walikamata pia baadhi ya vifaa vya kidijitali, baada ya waendesha mashtaka kutoa waranti wa kukamatwa kwa watu 216.

Rais wa Uturuki Recep Tayip ErdoganPicha: DHA

Duru hiyo imesema washukiwa waliokamatwa walituhumiwa kufadhili, kusajili na kueneza propaganda za PKK, kundi ambalo limeorodheshwa na Uturuki na nchi kadhaa za Magharibi kuwa la kigaidi.

"Matumizi mabaya ya madaraka na mbinu za vitisho kabla ya uchaguzi"

Emma Sinclair ambaye ni afisa wa kutetea haki za binadamu katika shirika la Human Rights Watch kanda ya Ulaya na Asia ya Kati amesema kupitia ukurasa wa Twitter kwamba vikwazo viliwekwa dhidi ya upatikanaji wa faili za uchunguzi, hatua anayosema "inadhihirisha wazi matumizi mabaya ya madaraka na mbinu za vitisho kabla ya uchaguzi".

Soma pia: Upinzani Uturuki waungana dhidi ya Erdogan

Chama cha tatu kwa ukubwa bungeni Uturuki HDP, kinakabiliwa na uwezekano wa kupigwa marufuku kufuatia kesi iliyowasilishwa dhidi yake kwenye mahakama ya kikatiba.

Kwenye kesi hiyo, chama hicho kinatuhumiwa kuwa na mafungamano na PKK, tuhuma ambazo kimekana.

Kutokana na hali hiyo, wagombea wake wanatafuta viti vya kisiasa kupitia muungano mdogo wa chama cha (Kijani Kushoto Green Left.

Kwa nini chama cha HDP kinampinga Erdogan?

Chama cha HDP si sehemu ya muungano wa upinzani. Lakini kinampinga vikali Erdogan baada ya misako ya miaka ya hivi karibuni dhidi ya wanachama wake, ambapo maelfu ya watu wakiwemo wabunge, mameya wamefungwa jela au wamevuliwa nyadhifa zao kwa madai ya kuwa na ufungamano naPKK.

Wanamgambo wa PKK walianzisha mapambano dhidi ya serikali ya Uturuki mnamo mwaka 1984 na zaidi ya watu 40,000 wameuawa kwenye machafuko hayo.

Chanzo: RTRE