Uturuki yazionya Iran na Urusi
10 Januari 2018Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema Iran na Urusi zinapaswa kutimiza wajibu wao na kuzuia mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya serikali ya Syria katika jimbo la Idlib liliko kaskazini mwa Syria. Uturuki imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Urusi na Iran katika juhudi za kumaliza mzozo wa Syria katika miezi kadhaa iliyopita, lakini imeongeza shinikizo kwa Urusi na Iran, kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi katika jimbo hilo.
Cavusoglu amesema Uturuki imekuwa ikichukua dhamana kwa vitendo vinavyofanywa na upinzani, hivyo ni jukumu la Urusi na Iran pia kufanya hivyo hivyo kwa upande wa serikali.
''Katika siku za hivi karibuni serikali ya Syria imefanya mashambulizi Idlib na mashariki mwa Ghouta. Jana tuliwaita wawakilishi wa Iran na Urusi na kuwapa onyo, kwa sababu katika makubaliano tuliyoyafikia, Urusi na Iran pia wanachukua dhamana kwa utawala wa Syria, kuuzuia usiendeleze mapigano pamoja na kuzuia ukiukaji wa haki za binadaamu,'' alisema Cavusoglu.
Amesema ukiukwaji huo hauwezi ukafanyika bila ya kuwepo msaada kutoka kwa Urusi na Iran. Urusi inataka kuzileta pamoja pande zinazohusika kwenye mzozo wa Syria katika mazungumzo yatakayofanyika Sochi, mwishoni mwa mwezi huu, lakini mvutano kati yake na Uturuki, unazusha wasiwasi. Lengo kubwa la mkutano huo ni kuanzishwa kwa katiba mpya baada ya kumalizika kwa vita Syria.
Wananchi wakimbia, wahitaji msaada
Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria vilivyodumu kwa takriban miaka saba, Uturuki imekuwa ikiwaunga mkono waasi wanaopambana na Assad, huku Urusi na Iran zikimuunga mkono Assad. Hata hivyo, licha ya tofauti hizo, Uturuki imeungana na mataifa hayo mawili yenye nguvu katika juhudi za kuleta amani ya kudumu nchini Syria, hata ingawa wachambuzi wameonya kwa muda mrefu kwamba ushirikiano huo wa pande tatu ni rahisi kuvunjika.
Ama kwa upande mwingine, Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binaadamu, Zeid Ra'ad al-Hussein amesema leo kuwa vikosi vya serikali ya Syria vimewaua kiasi ya raia 85 Disemba 31, 2017 katika mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya eneo linalodhibitiwa na waasi na ambalo limezingirwa. Miongoni mwa waliouawa ni wanawake 21 na watoto 30
Amesema hali katika eneo hilo linalokaliwa na raia wapatao 390, 000 ni sawa na janga la kibinaadamu na kwamba wakaazi wake wamekuwa wakishambuliwa kila siku kwa mashambulizi ya ardhini na anga, hali inayowalazimisha raia hao kujificha chini ya ardhi.
Waangalizi wameonya kuhusu janga la kibinaadamu, iwapo mashambulizi yataendelea Idlib, hasa kwa maelfu ya watu wasio na makaazi. Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Ulaya, kiasi ya watu milioni 1.4 wanahitaji msaada wa kibinaadamu katika jimbo la Idlib, huku zaidi ya 70,000 wakilikimbia eneo hilo kutokana na mapigano.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga