1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uundwaji wa kikosi cha DRC wakabiliwa na changamoto

Admin.WagnerD9 Oktoba 2012

Takribani mwezi tangu viongozi wa Kanda ya Maziwa Makuu kuridhia kuundwa kikosi cha kupambana na makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Lakini mpaka sasa uundwaji wake unakabiliwa na changamoto.

(L-R) South Sudan's President, Salva Kiir, Democratic Republic of Congo's President Joseph Kabila, Uganda's President Yoweri Museveni, and Tanzania's President Jakaya Kikwete talk during the Great Lakes Summit in Kampala on August 8, 2012. The summit opened today and will focus on security in Eastern Democratic Republic of Congo. AFP PHOTO/PETER BUSOMOKE (Photo credit should read PETER BUSOMOKE/AFP/GettyImages)
Mkutano wa Maziwa MakuuPicha: Getty Images/AFP

Hata hivyo kwa mujibu wa mawaziri wa Usalama katika kanda hiyo yapo matumani ya kikosi hicho kuanza kazi hivi karibuni. Hayo yanafuatia kikao kilichomalizika jana usiku mjini Kampala.

Nchi kumi 11 za Kanda ya Maziwa Makuu zimeteuwa timu ya maafisa kumi na 16 ambao shughuli yao itakuwa ni ukaguzi wa awali kwa lengo la kubaini mahitaji ya kikiosi hicho kinachokadiriwa kuwa na wanajeshi elfu nne kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa M23 na makundi mengine.

Mpaka sasa, Tanzania peke yake ndio iliyoahidi kutoa wanajeshi mara moja lakini kama waziri wa kigeni nchini Uganda Oryem Okello anasema kuna matumaini ya kupata wanajeshi wengine hivi karibuni. "Hatuna shaka hatuna shaka kuwa tutapata wanajeshi hao elfu nne. Angola imetuhakikishia kuwa inaunga mkono kuundwa kwa kikosi cha wanajeshi elfu nne ingawa hawajatwambia kama watatupa wanajeshi, nchi nyingine za kutoka kusini mwa Afrika nazo pia zimetwambia ziko tayari kutupa majeshi lakini zingali zinajadiliana". Alisema waziri huyo.

Mpiganaji muasi nchini KongoPicha: picture-alliance/dpa

Wakati majadiliano hayo yakiendelea, waziri Oryem Okello anaonesha matumaini ya kikosi hicho kuanza kazi katika siku za hivi karibuni.Ingawa hoja ya msingi inabakia kuwa ni lini? "Kile tulichokubaliana kwenye mkutano wetu ni kwamba kila kitu chafaa kutendeka kabla ya mwezi wa disemba kufika kati kati. Hapa tunazungumzia wanajeshi na vifaa watakavyohitaji". Alisema waziri Okelo.

Hivi sasa Kanda ya Maziwa Makuu inaomba msaada kutoka kwa Umoja wa Mataifa na umoja wa Afrika ili waweze kuwasaidia watu wa mashariki mwa Congo ambao wanakanbiliwa na tatizo la usalama kwa muda mrefu.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, Roger Meece ambaye anawaongoza wanajeshi elfu kumi na saba wa umoja huo ambao wanalinda amani Congo chini ya mwamvuli wa MONUSCO alisema "Tungependa kuunga mkono juhudi za nchi za ukanda wa maziwa makuu kadri tuwezavyo kulingana na majukumu na uwezo wa kifedha tuliyopewa na shirika la usalama la umoja wa mataifa".

Uganda kama taifa linalosifiwa katika kutoa wanajeshi wake katika ulinzi wa amani barani Afrika tayari imekwisha sema iko tayari kuchangia hata wanajeshi wote elfu nne kama itakubaliwa katika na nchi za maziwa makuu.

Kikao cha nne cha ukanda wa maziwa makuu kilimalizika mwendo wa saa sita jana usiku baada ya vuta ni kuvute kati ya nchi mbali mbali za ukanda wa maziwa makuu. Wajumbe walitofautiana kuhusu maswala fulani ambayo hakuna mjumbe aliyetaka kuyazungumzia.

Mwandishi:Leylah Ndinda
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi