1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine watimiza miaka miwili

24 Februari 2024

Leo imetimia miaka miwili tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine na kuzusha mzozo mkubwa ndani ya bara la Ulaya tangu Vita Vikuu vya pili vya dunia.

Wapiganaji wa Ukraine
Wapiganaji wa UkrainePicha: Ben Birchall/empics/picture alliance

Ilikuwa ni Februari 24, 2022, pale vikosi vya Urusi vilipovuka mpaka na kuanza kuishambulia Ukraine.

Rais Vladimir Putin alitoa hotuba ya kutetea uamuzi wake wa kuingia kijeshi Ukraine, akisema ilikuwa ni kwa maslahi ya utawala mjini Moscow na kujibu wasiwasi wake wa kiusalama kwa kile alichodai kwamba ni kujitanua kwa mataifa ya magharibi kuelekea Urusi.

Uvamizi huo ulijibiwa mara moja kwa viongozi wa mataifa ya magharibi kuulaani na kuapa kuihami Ukraine kadri inavyowezekana dhidi ya kile walikiita "vita vya Putin" na uonevu wa kiongozi huyo wa Urusi.

Miaka miwili baadaye msimamo huo wa nchi za magharibi inaonesha bado umesalia imara na viongozi kadhaa wamesafiri kwenda mjini Kyiv kuonesha mshikamano na Ukraine.

Mawaziri wakuu wa Italia, Canada na Ubelgiji, ambao ni Giorgia Meloni, Justin Trudeau na Alexander De Croo walisafiri kwenda nchini humo wakiwa pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, wakitokea Poland kwa njia ya treni.

Wamekutana na rais Volodomyr Zelensky na kujerea ahadi yao ya kuendelea bila kuchoka kuiunga mkono nchi hiyo kushinda vita dhidi ya Urusi.

Rais Zelensky aapa kutosalimu amri vita vinapoingia mwaka wa tatu

Kutoka kushoto Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, wa Italia, Giorgia Meloni, rais Volodomyr Zelensky, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Alexander De Croo wakiwa mjini Kyiv kwa maadhimisho ya miaka miwili ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, 24.02.2024.Picha: dpa

Akizungumza mjini Kyiv, rais wa Ukraine, Volodomyr Zelensky, ameapa kuishinda Urusi wakati vita vya nchini mwake vinaanza mwaka wa tatu.

"Tumepigana (vita hivi) kwa siku 730 za maisha yetu. Tutashinda katika miongoni mwa siku muhimu kabisa za maisha yetu," amesema Zelensky wakati wa mkusanyiko wa kuadhimisha miaka miwili ya vita uliofanyika mjini Kyiv.

"Mtu yeyote angetamani vita viishe. Lakini hakuna miongoni mwetu atakayeruhusu Ukraine isambaratike," amesema Zelensky, akitilia mkazo kwamba vita hivyo ni lazima viishe "chini ya masharti yetu, na kupata amani iliyo ya "haki".

Alikuwa akizungumza akiwa ameambatana na viongozi wa Canada, Italia, Ubelgiji pamoja na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.

Kwenye mkusanyiko huo Zelensky aliwakumbatia viongozi hao na kutoa nishani kwa wanajeshi.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwenye uwanja wa ndege wa Gostomel, ambao ulilengwa na vikosi vya Urusi mnamo siku za mwanzo za uvamizi.

"Miaka miwili iliyopita, tulikutana na vikosi vya adui vikitua hapa kwa mabavu, miaka miwili baadaye, tumekutana hapa hapa na marafiki na washirika wetu," amesema rais Zelensky.

Salamu za mshikamano zatolewa na viongozi wa nchi za magharibi

Katika siku ya leo ya maadhimisho, viongozi wa mataifa ya magharibi wametuma ujumbe wa mshikamano na Ukraine na ahadi za kuendelea kuiunga mkono nchini hiyo ishinde vita vinavyoendelea.

Miito ya kutaka vita hivyo vimalizwe imetandaa kila kona barani Ulaya katika maadhimisho ya miaka miwili. Wanaharakati wakiwa mjini Berlin kutuma ujumbe wa "komesha mauaji".Picha: Annette Riedl/dpa/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani amesema watu shupavu wa Ukraine wanaendelea na mapambano bila kuchoka kupigania uhuru na hatma yao. Amesema muungano wa kijeshi wa NATO umesalia imara na ulio na mshikamano kushinda wakati wowote ule.

"Na muungano usio mfano wa nchi 50 duniani unaoiunga mkono Ukraine, ukiongozwa na Marekani, umesalia na utarayi wa kuipatia msaada unaohitajika Ukraine na kuiadabisha Urusi kutokana na uchokozi wake," amesema Biden katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka miwili ya vita.

Rais Maia Sandu wa Moldova amewashukuru raia wa Ukraine kwa mapambano yao ya bila kuchoka kupigania uhuru na kulinda amani ya Moldova vilevile. Amesema katika miaka miwili, ulimwengu umeonesha mshikamano usio wa kawaida na kwamba kwa sababu vita havijamalizika ni lazima uungaji huo mkono uendelea kwa nguvu kubwa zaidi.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni ambaye yuko mjini Kyiv, amesema mji huo mkuu wa Ukraine ni alama ya kushindwa kwa Moscow na fahari ya Ukraine.

Kwa upande wake waziri mkuu wa Polandc, Donald Tusk amesema miaka miwili ya vita ni ya ushujaa wa Ukraine na ukatili wa Urusi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ametoa mwito wa kufufuliwa dhamira ya nchi za magharibi katika kuisaidia Ukraine kujihami. Amesema wakati huu ni wa kuonesha kwamba "utawala wa mabavu hauwezi kupata ushindi na kusema kwa mara nyingine kwamba tunasimama na Ukraine leo na hata kesho"

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW