Uwezekano wa kuachuliwa huru mateka watatu kutoka kwa waasi wa kikomunisti wa Colombia upo
27 Desemba 2007Kiongozi wa Venezuela-Hugo Chavez- asema uwezekano upo wa waasi wa Kimaksisti wa Colombia kuwaachilia huru mateka watatu baada ya serikali ya Colombia kukubali mpango wake wa kuwakabidhi aliokubaliana na waasi hivi karibuni.
Utawala wa Bogota, mji mkuu wa Colombia, umeukubalia mpango wa Chavez jana baada ya yeye Chavez, kusema kuwa hiyo ndio njia pekee inayohitajika kuanzisha operesheni ya kuwachukua mateka hao-wanawake wawili na mtoto mmoja kutoka kwa wapiganaji wanaojulikana kama –Revolutionary Armed Forces of Colombia- FARC.
Chavez, kabla ya kupewa ruhusa, alinukuliwa akiuomba utawala wa Colombia kushirikiana naye katika suala hili,akiongeza kuwa japo ana njia za siri zinazoweza kufuatwa ili kufikia lengo hilo lakini hakutaka kulitumia akisema lina ugumu wake.
Jamaa za mateka zilifurahi wakati Chavez alipotangaza hatua zake za kuwachukua mateka hao kutoka sehemu ya siri ndani ya Colombia.Miongoni mwa hao wanaotazamiwa kuachiliwa huru ni mbunge Consuelo Gonzalez de Pedro wa miaka 57; Clara Rojas-44 na Emmanul -3 mtoto wa Rojas aliemzaa na muasi wakiwa mateka.
Wanawake hao wamekuwa mateka tangu mwaka mmoja mwaka wa 2001 na mwingine mwaka wa 2002.
Rajas alikuwa msimamizi wa kampeini za mgombea urasi wa mwanasiasa Ingrid Betancourt wakati walipochukuliwa mateka na wapiganaji wa FARC mwezi Febuari mwaka wa 2002. Betancourt yeye anashikiliwa mateka.
Rojas na Betancourt ni miongoni mwa mateka 45,mkiwemo raia watatu wa Marekani ambao waasi wanataka kuwabadilisha na wanachama wa kundi la FARC wapatao 300 wanaoshikiliwa na serikali ya Colombia.
Hata hivyo pande hizo mbili hazijakubaliana na masharti ya jinsi ya kubadilishana watu hao.
Rais wa Colombia- Alvaro Uribe alimteua Chavez kama mpatanishi kati ya serikali na waasi hao na kutafuta njia za kubadilshana watu hao, lakini Chavez aliondolewa katika kazi hiyo na kiongozi wa Colombia baada ya Chavez kupuuza masharti kuwa asiwasiliane moja kwa moja na majenerali wake.
Licha ya hayo Chavez ameendelea na juhudi za mateka na kundi la FARC lilitangaza Disemba 18 kuwa litawaachilia huru mateka watatu kwa Chavez ama mjumbe wake atakae mchagua.
Chini ya mpango huo uliotolewa jana, ndege za Venezuela zitaelekea Colombia zikiwa na wajumbe kutoka Ufaransa, argentina,Brazil, Cuba, Bolivia, na Ecuador pamoja na wawakilishi wa chama cha msalaba mwekundu.Chavez atawakilishwa na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Ramon Rodriguez,huku colombia imemteua mjumbe wake wa masuala ya amani Luis Carlos Restrepo.