Uwezekano wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Madagascar ni mdogo
29 Aprili 2010Rais wa mpito nchini Madagascar, Andry Rajoelina, amesema kuna uwezekano mdogo wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kumaliza mzozo wa kisiasa katika kisiwa hicho, baada ya mazungumzo na mahasimu wake yaliyofanyika Pretoria, Afrika Kusini kukwama mapema leo. Akizungumza na waandishi habari mjini Pretoria, Afrika Kusini, kiongozi huyo wa mpito wa Madagascar, Andry Rajoelina, amesema kuwa kuna pengo kati ya ukweli na mkataba ambao tayari umeanzishwa. Kiongozi huyo ameongeza kuwa mazungumzo hayo yaliyokwama yataendelea tena baadae hii leo, lakini anadhani kuwa kuna nafasi ndogo sana ya serikali ya umoja wa kitaifa kuanzishwa na lazima ufumbuzi mwingine upatikane.
Viongozi wa kisiasa wanaohasimiana nchini Madagascar walikutana katika jitihada mpya za kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa ili kuliondoa taifa hilo kwenye mzozo wa kisiasa ulioanza nchini humo baada ya Rajoelina kumuondoa madarakani Rais Marc Ravalomanana, mwezi Machi mwaka uliopita wa 2009, huku akiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo. Mazungumzo hayo ni mfululizo wa mikutano baina ya Ravalomanana na Rajoelina na marais wa zamani, Didier Ratsiraka na Albert Zafy.
Awali Rajoelina, mwenye umri wa miaka 35, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa hawezi kukubaliana na baadhi ya matakwa ya Ravalomanana. Kiongozi huyo wa mpito ameongeza kusema kuwa yuko tayari kuunda serikali pamoja na makundi mengine ya kisiasa, likiwemo lile la marais wa zamani, kabla ya kufanyika uchaguzi nchini humo. Rajoelina amebainisha kuwa uchaguzi wa wabunge lazima ufanyike ndani ya miezi kadhaa na uchaguzi wa urais ufanyike mwezi Novemba.
Mahasimu hao wakutana na wapatanishi
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, mpatanishi kiongozi wa mzozo huo, Joaquim Chissano, na mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, jana walikutana kwa nyakati tofauti na viongozi hao wanne wa Madagascar. Viongozi hao wanne wa kisiasa tayari wamesaini mkataba wa kugawana madaraka, ambao baadae ulikiukwa na Rajoelina kwa kutotekeleza makubaliano hayo, jambo lililosababisha Umoja wa Afrika-AU, kuiwekea vikwazo serikali yake. Vikwazo vilivyowekwa na umoja huo ni pamoja na vile vya kiuchumi na marufuku ya kusafiri pamoja na kuzuia mali za viongozi wa serikali hiyo.
Mwezi Novemba, Rajoelina alisaini mkataba wa kumaliza mzozo wa kisiasa na Ravalomanana anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini pamoja na marais wengine wawili wa zamani katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Katika makubaliano hayo, Rajoelina ilikuwa aendelee kushikilia wadhifa wake kama rais, lakini akiwa na makamu wawili wa rais kutoka makundi mengine ya kisiasa. Hata hivyo, mkataba huo uligubikwa na matatizo kadhaa, ikiwemo kutokubaliana katika suala la kugawana madaraka hasa nafasi muhimu. Mzozo huo wa kisiasa katika kisiwa hicho kilichoko katika Bahari ya Hindi umesababisha kuzorota kwa hali ya kiuchumi na pia kuwafanya wawekezaji kutishia kujiondoa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)
Mhariri: Miraji Othman