1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzbekistan yaahidi kuisaidia Marekani kuchunguza ugaidi

1 Novemba 2017

Raia wa Uzbekistan ndiye mshukiwa wa shambulio lililouwa watu wanane New-York wakati watu wakiwa katika hekaheka za sherehe za Halloween nchini Marekani

USA New York Autoanschlag in Manhattan
Picha: Reuters/A. Kelly

Rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev amemwambia rais wa Marekani Donald Trump leo kwamba nchi yake iko tayari kutumia njia zote kusaidia katika uchunguzi wa shambulio lililosababisha vifo jijini New-York hapo jana wakati wa sherehe za sikukuu ya Halloween.Uzbekistan imetoa rambi rambi kwa Marekani kufuatia tukio hilo.Inatajwa kwamba mshambuliaji aliyeuwa watu wanane na kujeruhi wengine kadhaa  ni raia wa Uzbekistan.

Muda mfupi baada ya kutokea shambulio hilo rais wa Marekani Donald Trump alitowa ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twita na kutowa salamu za rambirambi kwa wahanga wa tukio hilo la kigaidi akisema pia Marekani haipaswi kuruhuhusu ISIS kurudi au kuingia nchini humo baada ya kuwashinda vitani katika eneo la Mashariki ya kati na kwengineko,imetosha. Ujumbe mwingine wa rais huyo ukaweka wazi kwamba ameitaka wizara ya usalama wa ndani kuimarisha zaidi mpango wa kuwahakiki wanaoingia nchini Marekani akisema kuchukua hatua sahihi za kisiasa ni suala zuri lakini sio kwa suala hili.

Usalama waimarishwa New-YorkPicha: Reuters/A. Kelly

Mtu anayetuhumiwa kufanya shambulio hilo lililowauwa watu wanane kwa kuvurumiza gari katika kati ya watu waliokuwa wakitembea kwenye barabara inayotumiwa na waendesha baiskeli na wanaokwenda kwa miguu anasemekana huenda alikuwa anafanya kazi ya udereva na akiishi katika mji wa New Jersey baada ya kuhamia nchini Marekani akitokea Uzbekistan miaka saba iliyopita,kwa mujibu wa ripoti zinazotolewa na maafisa na vyombo vya habari. Taarifa nyingine kuhusu mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 29 zimeibuka tangu hapo jana Jumanne mchana lilipotokea shambulio hilo la Manhattan  katika maeneo yaliyotokea mashambulizi ya Septemba 11 2001 ambayo yaliharibu kabisa jengo la kihistoria la kimataifa la biashara World Trade Center.Pia inatajwa kwamba aliwacha ujumbe akidai kwamba amefanya shambulio hilo la mauaji kwa niaba ya kundi la itikadi kali la dola la kiislamu kwa mujibu wa ripoti ambazo hazikuweza kuthibitishwa mara moja na shirika la habari la Reuters.Meya Bill  De Blasio amezungumza na waandishi habari na kutowa maelezo haya.

 

''Ni siku ya kuhuzunisha sana katika mji wetu,mkasa mbaya katika upande wa magharibi.Niwe wazi kwamba kutokana na taarifa tulizonazo kwa wakati huu,hili hiki kilikuwa kitendo cha kigaidi na hasa ni kitendo cha uoga cha ugaidi kilichowalenga raia wasiokuwa na hatia,kilichowalenga watu walikuwa katika shughuli zao za kimaisha,ambao hawakuwa na fikra yoyote kuhuusu kitakachowakumba.Sisi katika wakati huu kulingana na taarifa tulizonazo ni kwamba watu wanane wasio na hatia ndio waliopoteza maisha yao''

Picha: Reuters/A. Kelly

Polisi imekataa kabisa kutoa taarifa za mtu huyo lakini duru za karibu na uchunguzi unaonedelea zinamtaja mtu huyoaliyepigwa risasi na kukamatwa na polisi  kwamba anafahamika kwa jina la Sayfullo Habibullaevic Saipov na sio raia wa Marekani.Lakini hadhi yake ya uhamiaji bado haijafahamika wazi.Lakini kinachofahamika ni kwamba alizaliwa mwezi Februari mwaka 1988 na kuhamia nchini Marekani mwaka 2010 kutokea Uzbekistan nchi ambayo iko Asia ya Kati ambayo iliwahi kuwa sehemu ya Umoja wa kisovieti.Inavyoonekana aliwahi kuishi katika miji ya Ohio,Florida na New Jersey.Serikali ya Uzbekistan imeshasema hii leo kwamba imeanza kuchunguza ripoti kwamba raia wake ndiye muhusika wa shambulio hilo la kigaidi nchini Marekani lilowauwa watu wanane miongoni mwao wakiwa ni wanafunzi watano wakiargentina.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW