VALENCIA : Onyo juu ya athari ya mabadiliko ya hali ya hewa
17 Novemba 2007Repoti muhimu ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwepo kwa taathira za ghafla na zisizoweza kurekebishwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa iwapo hazitochukuliwa hatua za haraka kuzuwiya hali hiyo.
Jopo la Kiserikali juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa IPCC limetowa repoti yake hiyo mjini Valencia Uhispania leo hii baada ya mazungumzo ya muda mrefu miongoni mwa wajumbe wa serikali na wataalamu wa hali ya hewa.
Imesema kwamba harakati za binaadamu zinasababisha kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani na kwamba upunguzaji mkubwa wa gesi zenye kuathiri mazingira unahitajika kuepusha athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema serikali lazima zichukuwe hatua zaidi kupambana na mabadilioko ya hali ya hewa.
Amesema ujumbe uliomo uko wazi kabisa tishio la mabadiliko ya hali ya hewa ni la kweli na kuna njia madhubuti zinazowezwa kumudu kupambana na hali hiyo.
Jopo la IPCC linasema waraka wao huo utatumika kama muongozo na wanasiasa wanaokabiliwa na utowaji maamuzi juu upunguzaji wa uchafuzi wa hali ya hewa kutokana na nishati zinazoathiri mazingira,kutumia nishati safi na kuimarisha hatua za kupambana na mafuriko na majanga mengine ya asili ambayo yanatazamiwa kuwa makubwa zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.