1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Valerie Amos awasili Sudan Kusini

27 Januari 2014

mgogoro wa kibinadamu unaendelea kushuhuhudiwa Sudan Kusini huku waasi na serikali wakilaumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano ya kuumaliza mzozo huo.

Valerie Amos-Mkuu wa UN anayehusika na masuala ya msaada wa kibinadamu
Valerie Amos-Mkuu wa UN anayehusika na masuala ya msaada wa kibinadamuPicha: Ebrahim Hamid/AFP/Getty Images

Bibi Amos aliwasili mjini mkuu wa Sudan Kusini Juba akiianza ziara yake ya siku tatu katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kibinadamu kufuatia vita.Amos anatarajiwa jioni hii (Jumatatu 27.01.201)kukutana na maafisa wa serikali pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya misada katika juhudi za kujaribu kuimarisha misaada katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vilivyowafanya maelfu ya watu kuuwawa na wengine zaidi ya 700,000 kuyakimbia makaazi yao katika kipindi cha wiki sita za umwagikaji wa damu.

Mapigano nchini humo yamesababisha wimbi la matukio ya ulipizaji kisasi huku wapiganaji na makundi ya waasi wa kikabila wakitumia nguvu kuendesha visa vya uporaji. Halikadhalika ni kufuatia mapigano hayo Umoja wa Mataifa pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu wanasema kuna unyama mkubwa na mauaji ya kutisha yamefanywa na pande zote husika katika mgogoro huu.

Raia wa Sudan Kusini wanazidi kuitoroka nchi wakati mapigano yakiendeleaPicha: Reuters

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya misaada anatarajiwa pia kusisitiza juu ya umuhimu wa kuhakikisha ulinzi wa raia pamoja na wafanyakazi wa misaada. Ziara ya bibi Amos inakuja wakati kukiwa na mvutano na hali ya kutupiana lawama kati ya serikali na waasi huku kila upande ukimlaumu mwenzake kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha vita yaliyoanza kufanya kazi Ijumaa jioni.

Hata hivyo pande zote mbili zimesisitiza juu ya kujitolea kuunga mkono makubaliano hayo na kudai kwamba wamekuwa wakifyatuliana risasi kwa lengo la kila upande kujilinda.Msemaji wa jeshi Phillip Aguer amewashutumu waasi leo kwa kukiuka mara mbili makubaliano hayo ya kusimamisha vita.Aguer halikadhalika amesema kuna mashambulizi makubwa yaliyofanywa dhidi ya ngome zao siku ya jumapili ambapo yaliripotiwa mapigano katika eneo la kaskazini lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Upper Nile pamoja na jimbo la Jongeli mashariki ya nchi hiyo.

Riek Machar na Salva KiirPicha: Reuters

Kwa mujibu wa Aguer wanajeshi wake wanne wameuwawa katika mji wa Mathiang jimboni Jonglei na kwa upande wa jeshi hilo limelipiza kisasi na kuua kiasi waasi 120 ingawa hadi sasa haijawa rahisi madai hayo kuthibitishwa na vyombo huru.Itakumbukwa kwamba hapo jana (Jumapili 26.01.2014)waziri wa mambo ya nje wa Norway Borge Brende akizungumza kutokea Sudan alisema makubaliano ya kusitisha vita yanalegalega.Norway ni moja wapo ya nchi tatu za kigeni zenye dhima kubwa katika kuisaidia nchi hiyo changa barani Afrika,ikiwa pamoja na Uingereza na Marekani.Kundi la nchi 7 wanachama wa IGAD ndilo lenye jukumu la kusimamia utekelezwaji wa makubaliano hayo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed AbdulRahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW