1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VATICAN CITY : Dunia yaomboleza kifo cha Papa

3 Aprili 2005

Huzuni na sifa zimeitawala dunia leo hii kumkumbuka Baba Mtakatifu John Paul wa Pili ambaye kifo chake hapo jana usiku kimemaliza kipindi cha miaka 26 katika wadhifa wa upapa ambao umesaidia kuangusha ukomunisti barani Ulaya na mapambano ya kuwania amani duniani.

Kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 84 wa Wakristo wa madhehebu ya Katoliki bilioni moja na milioni moja duniani amefariki dunia saa tatu na dakika 37 usiku hapo jana baada ya kuwa mahtuti kwa siku mbili kutokana na viungo vyake muhimu moyo na mafigo kushindwa kufanya kazi pamoja na kukabiliwa na matatizo ya kupumuwa na magonjwa mengine kwa miezi miwili.

Kipeo cha huzuni kilikuwa katika uwanja wa St Peter makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Vatikani nje ya nyumba ya papa ambako watu walikuwa wakitiririkwa machozi huku makasisi watawa na umma wa wananchi wa kawaida wa Italia pamoja na wageni 100,000 waliofurika hapo wakiomboleza kwa sala.

Kifo cha Papa kimeibuwa huzuni isio ya kawaida duniani huku watu wa dini zote na wale wasiokuwa waumini wakitowa heshima zao kwa ubinaadamu,ushujaa na heshima yake ya uadilifu.

Akiongoza maombolezo ya Wamarekani Rais George W Bush wa Marekani amemsifu Papa kuwa ni mmojawapo wa viongozi waadilifu wakubwa katika historia.Rais Mohammad Khatami wa Iran akituma rambi rambi zake amesema Papa John Paul wa Pili alikuwa ni mtafutaji wa ukweli,haki na amani.Akiomboleza kifo hicho cha Papa Rais Mwai Kibaki wa Kenya amemuelezea kuwa ni mtu alieibadili dunia kuwa bora zaidi.

Zaidi ya makadinali 100 wameitwa mjini Rome Italia kumchaguwa mrithi wa Papa katika mkutano ambao kwa kawaida hufanyika baada ya siku 15 hadi 20 kufuatia kifo cha Papa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW