1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela yapuuzilia mbali vitisho vya Trump

Yusra Buwayhid
19 Julai 2017

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ametupilia mbali kitisho cha Rais wa Marekani Donald Trump cha kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi, iwapo serikali ya Maduro itaitisha uchaguzi wa kuiandika tena katiba.

Venezuela Nicolas Maduro
Picha: picture alliance/dpa/Sipa

Venezuela imekataa wito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha mpango wake wa kutaka kuiandika tena katiba ya nchi, ili kuimarisha nguvu ya serikali yake ya kisoshalisti. Akiwa katika mkutano wa dharura na Baraza la Usalama la Taifa aliouitisha baada ya wito wa Trump, na kuonyeshwa kwenye televisheni, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema serikali ya kigeni haiwezi kuidhibiti Venezuela. Maduro aliongeza kwamba nchini Venezuela, raia wa nchi hiyo ndiyo wenye uwezo wa kutoa amri na si Trump.

"Marekani inaitaka serikali ya Venezuela kuachana na pendekezo lake la Baraza la Taifa la Kutunga Katiba. Na Venezuela inaitikia hivi: Pendekezo la kuteua Baraza la taifa la kutunga katiba lipo kwenye mikono ya wananchi na ni raia walio huru wa Venezuela pekee wenye haki ya kupiga kura Julai 30 na si mtu mwengine yeyote," amesema Rais Nicolas Maduro.

Trump alitishia Jumatatu iliyopita kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Venezuela, iwapo Maduro ataendelea na uamuzi wake wa kuitisha kura ya kuteua baraza la katiba litakaloibadilisha katiba ya nchi. Wafuasi wa chama cha kisoshalisti wanataka Bunge limpe Maduro mamlaka zaidi juu ya taasisi chache ambazo bado hazipo chini ya udhibiti wa chama tawala.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Venezuela Samuel Moncada, amesema katika televisheni ya taifa kwamba uchaguzi wa kuteua wanachama wa baraza hilo utafanyika kama ulivyopangwa na kwamba Maduro amemtaka kufikiria tena mahuasiano ya kidiplomasia kati ya Venezuela na Marekani.

Maafisa wa serikali ya Trump wamewaambia waandishi habari hapo jana kwamba wanazingatia kuiwekea Venezuela vikwazo vipana zaidi, ikiwa ni pamoja na kusitisha biashara ya mafuta na nchi hiyo. Venezuela inaiuzia Marekani mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku, ikiwa ni nusu ya mauzo yake kwa nchi za nje.

Trump amewawekea vikwazo vya kusafiri na kukamata mali za maafisa kadhaa wa ngazi za juu katika wiki za hivi karibuni, lakini alijizuia kuiwekea vikwazo vikubwa zaidi nchi hiyo ambayo tayari imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Upinzani kwa uande wake Jumatatu iliyopita uliitisha mgomo wa masaa 24 nchini kote, wa kumshinikiza Maduro kuachana na mpango wake wa kuiandika tena katiba ya nchi. Upinzani umesema zaidi ya watu milioni 7.5 walipiga kura isiyo rasmi nchini kote Jumapili iliyopita, ya kupinga uchaguzi wa Julai 30, ulioitishwa na Maduro wa kuteua baraza la kubadilisha katiba ya nchi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/ap

Mhariri: Bruce Amani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW