Vettel ashinda mbio, Janga Bahrain
23 Aprili 2012Kiu cha Sebastiana Vetter kimekamilika baada ya kushinda mashindano haya akiwakilisha kampuni yake ya Red Bull. Wakati mashindano hayo yalipokuwa yakiendelea waandamanaji walitumia nafasi hiyo kuelezea ulimwengu juu ya mgogoro baina ya waandamanaji na utawala wa Bahrain chini ya familiya Al-Khalifa.
Mashindano hayo mwaka huu yalioingiwa na mtafaruku na kugeuka kuwa mchanganyiko wa burudani na janga kwa taifa hilo. Hapo awali mfalme Hamad aliyatakia kheri mashindano haya na kusema hii inaonyesha imani kubwa kwa taifa lao.
Mashindano ya magari ya Bahrain Grand Prix yapewa kisogo
Hali ikiendelea kuwa tete na waandamanaji wakiendelea na maandamano yao serikali hiyo ikasema inaunda tume huru kuchunguza kilichotokea, ikiwa ni pamoja na mauaji ya mtu mmoja ambapo waandamanaji walidai aliuawa na polisi. inasemekana alipigwa risasi akiwa juu ya paa la nyumbani kwake, Mfalme huyo akasema hali ya usalama itarudi hivi karibuni.
Waandamanaji waliyapa kisogo mashindano hayo lakini walitumia nafasi hiyo kuueleza ulimwengu wa kimataifa juu ya kinachoendelea katika taifa lao kwa kuwatumia waandishi wa habari za michezo waliofika kuripoti mashindano hayo ya mbio za magari.
Vijana wakiwa wameficha nyuso zao kwa vitambaa, wakibeba mabomu ya petroli walikuwa wakizunguka katika mji huo usiku kucha huku polisi wakitumia mabomu ya machozi na silaha kukabiliana na waandamanaji.
Waandamanaji hao wanadai kuwa mashindano ya magari ya Grand Prix ni ya kifahari na ni matumzi mabaya ya fedha za umma. Hali hii inayojirudia tena mwaka huu ilitokea mwaka jana ambapo waandamanaji walifanya maandamano kudai mabadiliko zaidi ndani ya utawala wa Bahrain.
Serikali ya Bahrain inawalaumu wanaharakati kuwa kitendo chao kimeonyesha taswira mbaya nje ya taifa hilo. Nchini humo kuna waislamu wa madhehebu ya Shia wakidai kukandamizwa na waislamu wa madhehebu ya Suni ambao ni wachache na ndiyo wenye mamlaka ya kiutawala.
Maandamano ya mwaka jana
Mwaka jana vyombo vya dola viliwaondoa waandamanaji hao ambao waliweka maskani pembezoni mwa barabara, sawa na hali inayotokea hivi sasa na watu 35 waliuawa wakiwemo wanajeshi .
Kulingana na taarifa ya tume maalumu iliyoundwa na serikali ya taifa hili imedai kuwa watu kadhaa waliokamatwa katika maandamano ya mwaka jana walipigwa wakati wakiwa rumande.
Vyama vya upinzani vikiwakusanya waislamu wa madhehebu ya Suni, Shia na pia waumini wa dini nyengine vinapigania kuwepo na mabadiliko ya kidemokrasia na kulipa mamlaka bunge kuunda serikali ili kumaliza utawala wa kimabavu wa familia ya Al-Khalifa.
Mwaka jana inadaiwa utawala wa Kifalme uliwaalika wanajeshi kutoka Saud Arabia kupambana na waandamanaji nchini Bahrain. Mpaka sasa watu zaidi 80 wamefariki kutokana na maandamano na mapambano na polisi na vifo vyote vinatokana na matumizi makubwa ya nguvu ya vyombo vya usalama. Serikali ilipoulizwa juu ya matukio hayo ikawaeleza wahanga kama ni wafanya fujo na wahuni tu wa mitaani.
Marekani imekuwa ikitoa matamshi kwa tahadhari kuhusu kinachoendelea Bahrain, kuhofia kuharibu uhusiano wake na falme hiyo pamoja na Saudi Arabia, ambazo ni washirika wa Marekani katika kuzuia kile wanachokiona kuwa ni ushawishi waIran katika eneo hilo.
Mwandishi:Adeladius Makwega/RPT-analysis.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman