Video iliovuja yafichua wauwaji, watumishi wa rais Assad
6 Juni 2022Baadhi ya wachambuzi waliotazama video hiyo, wanaishutumu serikali ya Assad kuhusika moja kwa moja kwa baadhi ya ukatili mbaya zaidi uliofanywa wakati wa vita.
Mwishoni mwa April 2022, moja wa waasi wa Syria walivujisha video ya mauaji ya Tadamon.
Familia nyingi za wasyria ziliitazama video hiyo, wakilenga kujua nini hasa kilichotokea kwa ndugu na jamaa zao waliotoweka.
Moja ya familia ambayo kijana wao alietambulika kwa jina la Waseem Siyam, ilsiema alitoweka katika mazingira tata akiwa katika shughuli yake ya kawaida ambayo ni kusafirisha unga wa ngano katika kiwanda cha mkate cha serikali.
Katika video hiyo Waseem mwenye umri wa miaka 34 alitambuliwa na jamaa zake, alipoonekana akiongozwa katika shimo lililojaa maiti huku akiwa amefumbwa macho yake, alirushwa kwenye shimo hilo na kupigwa risasi na kuuwawa.
Soma pia:Vita vya Syria vilisababisha vifo 3,700 mwaka wa 2021
Video iliyovuja ilirekodiwa Aprili 16, 2013, ikiwa ni siku chache baada ya kutoweka kwa Waseem. Inaonyesha wanaume wawili waliovalia sare waliwaua watu 41 kwa mtindo aliouwawa Waseem.
Vita vya Syria sasa vimekuwa vikiendelea kwa miaka 11, ambapo maovu mengi yamefanywa na pande zote zinazohusika katika mapigano hayo.
Wauwaji walifurahia kile wanachokifanya
video ya mauaji ya Tadamon, iliyorekodiwa katika eneo lililokuwa likidhibitiwa na serikali wakati huo, hata hivyo, inaonesha kwa uwazi ukatili usio na chembe ya utu ulioratibiwa.
Video inawaonesha wauwaji wanafurahia kazi yao, wakiua raia mchana kweupe na kujiona wako juu ya sheria.
walifanya uhalifu huo huku wakirekodi video na wakati mwingine hata kufanya mzaha kwenye video hiyo, swali la msingi linabaki,kwanini walirekodi uhalifu huo? je walitaka kutengeneza tuzo za kivita? au kuwaonesha wakuu wao kwamba walitekeza kazi kama ilivyopangwa?
Haijalishi ni sababu zipi, lakini kuna uwezekano hawakufikiria kuwa video hiyo ingeonekana hadharani.
Wasomi waliojitosa katika utafiti hatari wawabaini wauwaji
Profesa wa masomo ya mauwaji ya wayahudi ya holocaust na mauaji ya kimbari kutoka chuo kikuu cha Amsterdam Ugur Umit Ungor, ni miongoni mwa watu wa kwanza waliopata nakala ya video hiyo 2019.
Yeye na mwenzake waliweza kuwatambua wauwaji wawili kwenye video hiyo Najib al-Halabi, ambaye tayari amefariki.
Soma Pia:Mashambulizi ya Marekani Syria yadaiwa kuwajeruhi raia kadhaa
Alikuwa sehemu ya wanamgambo watiifu kwa Rais wa Syria Bashar Assad mwingine ni Amjad Youssef ambae ni afisa katika kikosi cha ulinzi wa rais Assad.
Ungor aliiambia DW kuchambua video ili kubaini wauaji haikuwa kama utafiti wa kawaida wa kitaaluma.
Waliazimia kufanya kile ambacho hadi sasa ni wachache wameweza kufikia,ikiwemo kuandaa vielelezo kwamba serikali ya Syria inahusika moja kwa moja kwenye baadhi ya ukatili mbaya zaidi uliofanywa wakati wa vita.
Mitandao ya kijamii ilivyotumika kusaidia utafiti
Annsar Shahhoud ambae alishirikiana na Ungor katika utafiti kwa kutumia akaunti za kughushi kwenye mitandao ya kijamii ili kubaini ukweli wa mauaji.
akitumia jina la kike huku akionesha kumuunga mkono rais Assad alifanikiwa kuaminika na wafanyakazi wa Assad ambapo kwa njia ya simu aliongea na Amjad Youssef ambae alimwambia anahisi upweke na msongo wa mawazo.
katika mfululizo wa mazungumzo miezi kadhaa baadae alimwambia "aliuwa watu wengi." Hii ni katika mazungumzo ya simu ambayo yalisikilizwa moja kwa moja kwa siri na Ungor ambayo yalikamilisha utafiti wao.
Utafiti wafikishwa kwa waendesha mashtaka
Wasomi hao wawili hatimaye walikuwa wamefikia lengo la utafiti na kuwasilisha mazungumzo hayo yaliorekodiwa kwa waendesha mashtaka wa Uholanzi na Ujerumani.
Soma pia:Amnesty: Wanaorudi Syria wanateswa na kubakwa
Alexander Schwarz, mtaalamu wa sheria za kimataifa za uhalifu wa shirika la Amnesty International anasema,mashambulizi ya kimfumo kwa raia, kama inavyoonekana kwenye video, ni kigezo mojawapo cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Bado haijajulikana endapokesi itafunguliwa baada ya ufichuaji huo. Hukumu ya kifungo cha maisha iliotolewa kwa kwa mmoja wa afisa wa Syria Anwar Raslan na mahakama ya Ujerumani huko Koblenz mwezi Januari, inaonesha kwamba muuaji alienusurika kwenye video anaweza kufunguliwa mashtaka.