VIENNA: Makubaliano hayajafikiwa kuhusu hali ya baadaye ya Kosovo
22 Februari 2007Serikali ya Serbia na Walbania walio wengi katika jimbo la Kosovo, bado hawajakubaliana juu ya mpango wa Umoja wa Mataifa unaohusu hali ya baadaye ya mkoa huo wa Serbia.
Mpango uliopendekezwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, Matti Ahtisaari, unataka jimbo la Kosovo liwe huru kutoka kwa Serbia na liwe chini ya uangalizi wa jumuiya ya kimataifa. Mpango huo hata hivyo hautaji ikiwa jimbo hilo litakuwa na uhuru kamili na kuwa taifa.
Kufuatia mkutano wa jana mjini Vienna kuujadili mpango huo pamoja na pande hizo mbili, Ahtisaari ameondoa uwezekano wa kufikia maendeleo mapya kwa haraka.
Jimbo la Kosovo limekuwa chini ya utawala wa Umoja wa Mataifa tangu kampeni ya mashambulio ya mabomu iliyofanywa na shirika la kujihami la kambi ya magharibi, NATO, iliyomaliza vita vya kimbari mnamo mwama wa 1999.