Vienna. Mpango wa kinuklia wa Korea ya kaskazini hatimaye kufungwa.
9 Julai 2007Matangazo
Shirika la kimataifa la nishati ya Atomic limesema kuwa linapanga kutuma kikosi cha wachunguzi nchini Korea ya kaskazini baadaye wiki hii ili kuangalia ufungaji wa mpango wa kinuklia wa nchi hiyo.
Wanadiplomasia wanasema kuwa ujumbe huo ni lazima kwanza uidhinishwe na bodi ya shirika hilo lenye wanachama 35, ambao wanafanya kikao maalum leo Jumatatu mjini Vienna. Mkuu wa shirika hilo la umoja wa mataifa Mohamed el- Baradei amesema kuwa hatua ya kutuma ujumbe huo ni muhimu.
Suala la gharama za ujumbe wa uangalizi kwa ajili ya Korea ya kaskazini pia linapaswa kuamuliwa. Wanadiplomasia wanasema kuwa ujumbe huo utagharimu kiasi cha dola milioni 5 katika muda wa miaka miwili, na kwamba Marekani iko tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha hizo.