VIENNA: Uchunguzi wa vinu ya nyuklia kuanza tena Korea Kaskazini
14 Februari 2007Shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, limesema litaanzisha tena uchunguzi nchini Korea Kaskazini kufuatia hatua ya serikali ya mjini Pyongyang kutangaza itakifunga kinu chake cha nyuklia katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Kiongozi wa shirika hilo, Mohammed El Baradei, ameieleza hatua ya Korea Kaskazini kama hatua inayofaa kuumaliza mgogoro wa nyuklia wa nchi hiyo.
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Korea Kaskazini kukivunja kinu chake cha nyuklia waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice amesema uamuzi wa Korea Kaskazini ni ishara nzuri.
´Kufungwa kwa vinu vya nyuklia ni ishara kwamba wananchi wa Korea Kaskazini huenda wako tayari kufanya chaguo muhimu. Sitaichukulia hatua hiyo kama ishara kamili mpaka tuone wamefanya walivyosema, lakini bila shaka uamuzi wao ni hatua muhimu ya kusonga mbele.´
Naye waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair alikuwa na maoni haya kuhusu makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya mataifa sita hkuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.
´Kwa hiyo kilichotokea leo na Korea Kaskazini kinaonyesha tunaweza kufanikiwa. Lakini ni muhimu kutambua kwamba tumefaulu kwa sababu ya kuwa msimamo imara wakati wa majadiliano.´
Korea Kaskazini iliwatimua wachunguzi wa shirika la IAEA miaka minne iliyopita baada ya kukosolewa na Marekani kwamba ilitaka kutengeneza bomu la nyuklia. Wakati huo, Korea Kaskazini ilijiondoa kutoka kwa mkataba wa kimataifa wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia.