VIENNA. Waandishi walio uhamishoni kutunukiwa tuzo.
29 Aprili 2005Taasisi ya kimataifa ya vyombo vya habari IPI inatrajiwa kukitunukia kituo cha radio cha SW Radio Africa cha Zimbabwe katika dhifa ya kimataifa itakayo fanyika mjini Nairobi Kenya tarehe 24 mwezi wa tano.
Gerry Jackson muasisi na msimamizi wa kituo cha SW Radio Africa atapokea tuzo hiyo yenye heshima tele kwa wanahabari kwa jinsi kituo hicho kinavyo jikakamua kutoa habari nchini Zimbabwe ambako uhuru wa wanahabari unadhibitiwa na utawala wa rais Robert Mugabe.
Hadi leo vyombo huru vya habari ikiwa ni pamoja na gazeti pekee la Daily News nchini Zimbabwe vimefungwa.
Kituo hiki cha radio kimeweza kuendeleza matangazo yake kutoka nchini uingereza na kinaendeshwa na wanahabari wa Zimbabwe ambao wako uhamishoni nchini humo.
Gerry Jackson ni mwana habari mwenye ujuzi wa zaidi ya mika 25 ambae alifutwa kazi kutoka shirika la habari la Zimbabwe ZBC baada ya kupeleka hewani maoni ya wananchi kufuatia vurugu za kugombania chakula katika mji wa Harare mwaka wa 1997.