Vifaru vya Israel vyaingia rasmi Jiji la Gaza
19 Septemba 2025
Vifaru vya jeshi la Israel vilianza kuingia kwenye Jiji la Gaza siku ya Alkhamis (Septemba 18), huku huduma za intaneti zikikatwa,ikiwa ishara kwamba kungelikuwa na mashambulizi makali ya ardhini baada ya hapo.
Wakaazi wapatao milioni moja wanaoishi kwenye kitovu hicho cha Ukanda wa Gaza wanaripotiwa kukwama baina ya kukimbia na kubakia.
Wakati picha za video mitandaoni zikiwaonesha baadhi wakibeba mizigo yao wakiwa njiani kuelekea upande wa kusini mwa Gaza, kuna pia za wengine maelfu wanaosema hawaoni haja ya kuondoka kwa kuwa "ndani ya Ukanda mzima hakuna mahala palipo salama," huku njaa na mauaji yakiwanyemelea kila wendapo.
Awali, jeshi la Israel lilikuwa limedondosha vipeperushi ya kuwataka watu wote kuondoka kwenye jiji hilo, huku msemaji wa jeshi hilo anayetumia lugha ya Kiarabu, Avichay Adraee, akitowa tangazo lililowapa wakaazi hao hadi mchana wa Ijumaa (Septemba 19) kuwa wawe wameshaondoka.
Adraee alisema ili kuwezesha uhamaji kuelekea kusini, njia ya muda ilikuwa imefunguliwa kupitia Mtaa wa Salahaddin.
"Munaweza kupitia mtaa huo kuelekea Wadi Gaza kuanzia saa sita mchana wa Jumatano hadi saa sita mchana Ijumaa. Watu wapitie tu njia zilizowekwa alama ya njano na tafadhalini fuateni maelekezo ya vikosi vya usalama na alama za barabarani." Alisema msemaji huyo akisisitiza kwamba wakaazi wa Jiji la Gaza walikuwa wanapaswa "kuitumia fursa hii."
Hamas yatowa msimamo
Kwa upande wake, tawi la kijeshi la Hamas, Al-Qassam Brigade, lilitowa tamko kali likiapa kuendelea kukabiliana na wanajeshi wa Israel na kuwaonya kwamba operesheni "inayoendelea sasa haitaweza kuwaokowa mateka waliosalia."
Kupitia ujumbe waliouchapisha kwa lugha ya Kiabrenia siku ya Alkhamis, kundi hilo limesema Jiji la Gaza "litakuwa kaburi la wanajeshi wa Israel," ambapo wapiganaji wengi wenye silaha walikuwa wameshasambazwa kote kukabiliana nao, na kwamba sasa Israel ilikuwa imeamua yenyewe kujiingiza kwenye "vita vya kujimaliza vyenye gharama kubwa."
"Mateka wa Kiisraeli sasa wamechawanywa kwenye viunga vya Jiji la Gaza, na Al-Qasam Brigade haitaweza kuwalinda madhali Netanyahu ameamua kuwauwa." Ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, siku ya Ijumaa Israel ililifunga lango pekee linalouunganisha Ukingo wa Magharibi na Jordan, ikiwa ni siku moja tu baada ya dereva mmoja aliyekuwa akipeleka msaada wa kibinaadamu kutoka Jordan kwenda Gaza kuwauwa wanajeshi wawili wa Kiisraeli kwa risasi.
Hakuwa na kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo kwenye Daraja la Allenby, ambayo ni njia kuu ya biashara kati ya Jordan na Israel na lango pekee kwa zaidi ya Wapalestina milioni tatu wa Ukingo wa Magharibi kuifikia Jordan na sehemu nyengine za dunia.