1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifaru vyazidi kuingia ndani ya vitongoji vya mji wa Gaza

28 Septemba 2025

Magari ya kijeshi ya Israel yameendelea kuingia ndani ya vitongoji vya Gaza City, yakilenga maeneo ya Sabra, Tel Al-Hawa, na Al-Naser.

Gaza City | Ukanda wa Gaza 2025 | Mashambulizi ya Israel
Gaza city ikiwa chini ya mashambulizi ya vikosi vya Israel ikilenga kutokomeza kabisa kundi la HamasPicha: Khames Alrefi/Anadolu Agency/IMAGO

Mashahidi wanasema mamia ya maelfu ya raia bado wamekwama, huku mamlaka za afya zikishindwa kujibu maombi ya uokozi. Jeshi la Israel limesema limeshambulia maeneo 140 ya kijeshi katika saa 24 zilizopita, ambapo watu 21 wameuawa.

Wakati huo huo maandamano makubwa yamefanyika katika miji mbalimbali ya Israel, ikiwemo Tel Aviv na Jerusalem, wanakoendelea kuweka kambi karibu na makaazi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, wakishinikiza kukomeshwa kwa operesheni ya Gaza na kuachiwa kwa mateka.

“Familia za mateka zinaomba makubaliano na pia dunia nzima imechoshwa na vita. Hata Waisraeli pia wamechoshwa na vita. Kwa hiyo watu wanataka kuona hili likiisha. Na nafikiri njia pekee ya kumaliza ni kufikia makubaliano yatakayohakikisha usalama, yatakayohakikisha mustakabali bora kwa kila mtu. Na zaidi ya yote yatakayowarejesha nyumbani mateka wetu.”

Mashirika ya afya ya kimataifa yameonya hali ya kibinadamu inazidi kuzorota, huku hospitali kadhaa zikifungwa na mamia ya maelfu ya watu wakiendelea kuikimbia Gaza City.

Shirika la Chakula Duniani linakadiria kuwa hadi watu 400,000 wamekimbia Gaza City, lakini maelfu wengine bado wamekwama kwenye jiji hilo linalozingirwa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW