1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchafuzi wa hewa wasababisha vifo 1,200 kwa mwaka Ulaya

8 Mei 2023

Shirika la mazingira la Umoja wa Ulaya limesema kuwa uchafuzi wa hali ya hewa barani humo unaendelea kusababisha vifo 1,200 kwa mwaka.Wanaoathirika zaidi ni watoto na hilo huongeza hatari ya kupatwa na magonjwa sugu.

Symbolbild Luftverschmutzung in Europa
Picha: NIKOLAY DOYCHINOV/AFP/Getty Images

Licha ya maboresho yaliyofanywa katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha vichafuzi muhimu vya hali ya hewa katika nchi nyingi za Ulaya bado kiko juu ya miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), haswa katika Ulaya ya Kati na Italia.  Hayo yamesemwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Ulaya (EEA) baada ya kufanya utafiti katika zaidi ya nchi 30, ikiwa ni pamoja na zile 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.     

Hata hivyo, ripoti hiyo haikuangazia hali ilivyo katika mataifa makubwa ya kiviwanda kama Urusi, Ukraine na Uingereza, jambo linaloashiria kuwa idadi ya vifo barani Ulaya kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa inaweza kuwa kubwa zaidi.

EEA ilitangaza mwezi Novemba mwaka jana kuwa katika Umoja wa Ulaya, watu 238,000 walikufa mapema kwa sababu ya uchafuzi wa hali ya hewa mnamo mwaka 2020, idadi hiyo ikijumuisha pia mataifa ya Iceland, Liechtenstein, Norway, Uswisi na Uturuki.

  Soma pia: Magari yaliotumika yanachafua hali ya hewa katika mataifa yanayoendelea    

Shirika hilo limeendelea kusema kuwa uchafuzi wa hali ya hewa husababisha vifo vya mapema zaidi ya 1,200 kwa mwaka kwa watu walio chini ya umri wa miaka 18 barani Ulaya na huongeza hatari ya magonjwa sugu hapo baadaye maishani. Utafiti huo ulikuwa wa kwanza wa shirika hilo kuwalenga zaidi watoto.

EEA imeendelea kubaini kuwa ingawa idadi ya vifo vya mapema kwa watoto ni ndogo ikilinganishwa na idadi jumla ya watu wa bara la Ulaya inayokadiriwa na EEA kila mwaka, vifo hivi vya mapema ni hasara kubwa kwa mustakabali wa bara hilo, lakini pia magonjwa sugu yanayowakabili watoto ni mzigo mkubwa.

Shirika hilo limezitaka mamlaka kuzingatia uboreshaji wa hali ya hewa karibu na shule na chekechea pamoja na kuzingatia utengenezaji wa miundombinu ya michezo na vituo vya usafiri wa umma.

      

Kiwanda cha uzalishaji wa nishati ya umeme nchini Ujerumani huko Bergheim.Picha: S. Ziese/blickwinkel/IMAGO

Baada ya mtoto kuzaliwa, uchafuzi wa hali ya hewa unaomzunguka humuongezea hatari ya kupatwa na matatizo kadhaa ya kiafya, ikiwa ni pamoja na pumu, matatizo ya mzio, kupungua kwa kazi ya mapafu na magonjwa ya kupumua.

Hali mbaya ya hewa huweza pia kuongeza hatari ya magonjwa sugu kama vile pumu, ambayo huathiri asilimia tisa ya watoto na vijana barani Ulaya, na huongeza hatari ya kupatwa magonjwa sugu baadaye katika utu uzima.

 Soma pia:   Ripoti: Vichanga nusu milioni wafa kwa uchafuzi wa hewa 2019   

Kulingana na takwimu zilizotolewa hivi karibuni, mwaka 2021, asilimia 97 ya wakazi wa mijini waliishi katika mazingira ambayo viwango vya hali ya hewa havikukidhi mapendekezo ya Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO).      

Shirika la EEA mwaka jana ilisisitiza kwamba Umoja wa Ulaya ulikuwa kwenye muelekeo wa kufikia lengo lake la kupunguza vifo vya mapema kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 ikilinganishwa na mwaka 2005.

      

Mapema miaka ya 1990, chembechembe za gesi chafu zilisababisha karibu vifo milioni moja vya mapema kwa mwaka katika mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya. Hiyo ilishuka hadi 431,000 mnamo 2005.

Hali bado ni nzuri barani Ulaya ukilinganisha na sehemu zingine

Shirika la WHO inasema hali barani Ulaya inaonekana kuwa nzuri zaidi ukilinganisha na sehemu kubwa duniani. Uchafuzi wa hali ya hewa husababisha vifo vya watu milioni saba duniani kote kila mwaka, ikiwa inashabihiana na vinavyotokana na uvutaji sigara au lishe mbaya.

Soma pia: Oxfam: Matajiri wachache wanaathiri masikini kwa uchafuzi wa hali ya hewa     

Maelfu kadhaa ya vifo vinahusu watoto chini ya miaka 15. Ilibidi kusubiri hadi Septemba mwaka 2021 kufikia makubaliano ya kuimarisha sheria ya mwaka 2005 kuhusu uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa.

      

Mwanamume akivaa barakoa huko Chiang Mai, Thailand ili kujilinda na uchafuzi wa hali ya hewa.Picha: Pongmanat Tasiri/Zuma/IMAGO

Nchini Thailand pekee, ambako moshi wenye sumu huripotiwa sehemu mbalimbali za nchi hiyo, maafisa wa afya walisema wiki iliyopita kuwa watu milioni 2.4 walikuwa wameshapatiwa matibabu hospitalini kutokana na matatizo ya kiafya yanayohusishwa na uchafuzi wa hali ya hewa tangu mwanzoni mwa mwaka.

      

Chembe chembe ndogo za moshi mchafu, hasa kutoka kwenye magari na malori na ambazo zinaweza kupenya hadi ndani ya mapafu, zinachukuliwa kuwa kama uchafuzi mbaya zaidi wa hali ya hewa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW