1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo Indonesia kufuatia mripuko wa volkano sasa ni 34

John Juma
7 Desemba 2021

Idadi ya waliokufa pamoja na wale ambao bado hawajulikani waliko inatarajiwa kuongezeka kadri shughuli za uokozi na kufukua vifusi zinavyoendelea.

Indonesien Vulkanausbruch auf Java
Picha: Willy Kurniawan/REUTERS

Rais wa Indonesia Joko Widodo siku ya Jumanne amewatembelea waathiriwa wa mlipuko mkubwa wa volkano ambao ulisababisha vifo vya watu wasiopungua 34 na kuwaacha maelfu bila makaazi.

Widodo ameahidi kuwa waathirwa hao watajengewa makaazi mapya.

Mawingi ya majivu ya moto yalitanda angani huku gesi hatari na tope la moto pia vikitapakaa kwenye miteremko ya mlima Semeru umbali wa kilomita 11, baada ya volcano hiyo kulipuka siku ya Jumamosi kufuatia mvua kubwa.

Vijiji na miji midogo iliyoko karibu ilifunikwa na vifusi kutokana na volkano hiyo.

Rais Joko Widodo alitembelea êneo hilo la mkasa wilaya ya Lumajang, mashariki mwa mkoa wa Java kuwahakikishia waathiriwa kwamba serikali yake inawajali haswa wakati huu wakiwa na mahitaji makubwa ya msaada.

Ahadi ya misaada kwa waathiriwa

Baada ya kuwatembelea waathiriwa hao ambao wako katika kambi kwenye uwanja wa michezo, aliahidi kujenga upya miundo msingi ikiwemo daraja linalounganisha Lumajong na miji mingine. Aidha aliahidi kuondoa zaidi ya majengo 2,000 karibu na maeneo hayo hatari kutokana na volkano.

Waokoaji wanaendelea kutafuta watu ambao hawajulikani waliko baada ya mlipuko huo wa volkanoPicha: Zabur Karuru/Antara Foto/REUTERS

Awali, maafisa wa serikali walisema wakaazi ambao vijiji vyao vimeathiriwa watahamishwa kwa muda wa miezi sita ijayo, na kila familia itakayojengewa nyumba mpya pia itapewa dola 35 kila mwezi kama fidia.

Msemaji wa mamlaka inayoshughulikia majanga na masuala ya dharura Abdul Muhari alisema watu 56 walilazwa hospitalini wakiwa na majeraha ya kucbhomeka kutokana na mlipuko huo.

Alisema waokoaji wangali wanawatafuta wanakijiji 17 ambao bado hawajulikani waliko. ”Takriban nyumba 3,000 pamoja na shule 38 ziliharibiwa,” amesema Muhari.

Idadi ya vifo yaongezeka

Idadi ya waliokufa pamoja na wale ambao bado hawajulikani waliko inatarajiwa kuongezeka kadri shughuli za uokozi na kufukua vifusi zinavyoendelea.

”Operesheni ni ngumu kwa sababu ya eneo hilo kuwa la milima na miteremko,” amesema Andris Rufianto Putro alipokuwa akizungumza na shirika la Msalaba Mwekundu la Indonesia.

Mnamo Jumanne, timu yake ya uokozi ilifukua miili mitano iliyofunikwa kwenye vifusi vya nyumba Eneo la Renteng na miili mingine miwili pia iligunduliwa mkabala na Eneo hilo. Miili yote ilikuwa imechomeka. Katika kijiji jirani cha Supiturang, miili mingine mitano iligunduliwa.

Vijiji kadhaa vimeathiriwa na mripuko huo. Wataalam wametahadharisha kuhusu uwezekano wa gesi hatari kutokea.Picha: Trisnadi/AP Photo/picture alliance

Rufianto Putro amesema baadhi ya maeneo yanaweza kufikiwa tu kwa kutumia magari maalum mfano Hagglund yanayoweza kupita katika maeneo yenye mashimo, na mawe makubwa.

Ndege zilizobeba misaada kama vyakula, mahema, mablanketi na misaada mingine zilipeleka misaada Jumanne kwa takriban waathiriwa 3,700 ambao wamepoteza makaazi yao.

Soma Tsunami yaua 40, yaharibu majengo 600 Indonesia

Wataalam wametahadharisha kuwa huenda kukatokea maporomoko zaidi kufuatia mripuko huo wa volkano kwenye mlima wa urefu wa mita 3,676 na gesi hatari zinaweza kuwaathiri watu.

Shughuli za uokozi na kutafuta wasiojulikana waliko

Wayan Suyatna ambaye anaongoza shughuli za uokozi amesema timu yake imelenga zaidi maeneo matatu ikiwemo kijiji cha Sumberwuluh ambacho kiliathiriwa zaidi. Inaaminika watu wamekwama ndani ya majumba yao ambayo yalifunikwa hadi kwenye mapaa.

Baadhi ya majengo na hata magari yalifunikwa na majivu kutokana na mripuko huo wa Jumamosi.Picha: Trisnadi/AP Photo/picture alliance

”Majivu kutokana na mlipuko huo bado ni moto na kadri wanavyozidi kuchimba na kufukua ndivyo joto linazidi kuongezeka,” Amesema Suyatna.

Katika kipindi cha miaka 200 iliyopita, volcano ya Semeru, ambayo pia inajulikana kama Mahameru, imeripuka mara kadhaa.

Soma: Idadi ya watu waliokufa Indonesia yaongezeka hadi 1,407

Kando na Semeru, kuna volkano nyingine 129 ambazo pia huripuka nchini Indonesia.

Indonesia ambayo ina zaidi ya watu milioni 270 hukumbwa na matetemeko ya ardhi pamoja na miripuko ya volkano kwa sababu iko sambamba na êneo liitwalo kuwa "Ring of Fire” ambalo linakumbwa na shughuli asilia ya chini ya ardhi inayosababisha matetemeko na miripuko.

(APE)