1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Vifo kutokana na mafuriko vyafikia 2,300 Libya

Josephat Charo
12 Septemba 2023

Watu wapatao 2,300 wamekufa na maalfu wengine hawajulikani waliko nchini Libya kufuatia mafuriko makubwa yaliyovunja mabwawa na kusababisha uharibifu mkubwa katika mji wa Derna mashariki wa nchi hiyo.

Libyen Zerstörung nach Sturm Danial
Picha: Omar Jarhman/REUTERS

Huku hali ya wasiwasi ikiugubika ulimwengu, nchi kadhaa zimeahidi kutuma msaada wa dharura na timu za uokozi kuisaidia Libya ambayo inalemewa na kile ambacho afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amekieleza kuwa ni "janga la viwango vikubwa visivyo mithili".

Uharibifu mkubwa umetokea katika mji wa bandari wa Derna katika bahari ya Mediterania, uliokuwa nyumbani kwa wakazi 100,000, na ambako majengo kadhaa marefu ya ghorofa yalianguka na nyumba na magari kutoweka yaliposombwa na maji. Shirika la utoaji huduma za dharura la Libya limeripoti kwamba idadi ya vifo imefikia zaidi ya 2,300 mjini Derna pekee na watu zaidi ya 5,000 bado hawajulikani waliko, huku watu kiasi 7,000 wakiwa wamejeruhiwa.

Osama Ali wa shirika la Uokozi na huduma za dharura amesema hali mjini Derna inatisha na ni ya kushangaza mno, na ametoa wito msaada zaidi utolewe kuokoa maisha kwa sababu watu wangali wamesana chini ya vifusi na kila dakika ni muhimu.

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi amesema katika kauli yake iliyooneshwa kwenye runinga kwamba jeshi litapeleka vifaa na maafisa wake kwa ushirikiano na vikosi vya Libya kuzisaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko.

"Kuhusu Libya naamini tunatakiwa tuchukue hatua haraka kwa sababu ya ukubwa wa uharibifu. Kutokana na taarifa tunazopata tunatakiwa tusaidia na uwezo wetu wote na nafahamu kwamba kupitia uwezo wa jeshi tutashirikiana na jeshi la Libya."

Uturuki yapeleka msaada Libya

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake itasimama na Libya wakati nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ikikabiliana na changamoto za mafuriko. Akizungumza kwenye warsha mjini Ankara, Erdogan pia amesema idadi ya vifo kutokana na janga hilo inatarajiwa kuongezeka.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: Mustafa Kamaci/AA/picture alliance

"Nawaombea rehema za Mungu ndugu zetu waliopoteza maisha kwenye mafuriko Libya. Taarifa tulizopokea zinaonesha janga kubwa la asili limetokea. Kwa bahati mbaya inaonekana idadi ya vifo itaongezeka pamoja na idadi ya watu wasiojulikana waliko. Kama Uturuki, tunasimama na ndugu zetu na nyenzo zetu zote wakati wa siku hizi ngumu."

Jeshi la Uturuki limetuma ndege tatu zilizobeba timu za uokozi kutoka kwa wakala wa kitaifa wa kukabiliana na majanga na hali za dharura kwenda Libya.

Soma pia: Kamati ya uokoaji ya taifa na mawaziri wamelitembelea eneo la Derna

Mkuu wa Muungano wa kimataifa wa shirika la msalaba mwekundu na hilal nyekundu, IFRC, Jagan Chapagain, amesema wafanyakazi watatu wa kujitolea wa shirika la Msalaba Mwekundu wamekufa wakati walipokuwa wakiwasaidia wahanga wa mafuriko mashariki mwa Libya. Wafanyakazi hao wamekufa walipokuwa kazini wakizisaidia familia zilizonasa kufuatia kimbunga Daniel.

Waziri wa mambo ya nje wa Italia, Antonio Tajani amesema Italia itatuma msaada nchini Libya. Tajani ameandika katika mtandao wa X kwamba serikali ya Italia inachukua hatua ya haraka kufuatia miito ya kutolewa kwa msaada kwa ajili ya wahanga mashariki mwa Libya. Pia amesema timu maalumu itakayofanya tathmini iko njiani, ikiratibiwa na kikosi cha ulinzi wa umma.

Waziri wa ulinzi wa Italia Guido Crosetoo naye pia ameandika katika mtandao wa X kwamba ametoa msaada kutoka kwa jeshi kwa jili ya maeneo yaliyokabiliwa na mafuriko.

Kimbunga Daniel ambacho kiliua watu wapatao 27 wakati kilipopiga sehemu za Ugiriki, Uturuki na Bulgaria siku chache zilizopita, kilipiga mashariki mwa Libya Jumapili mchana.

(afp)

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi