Vifo kutokana na virusi vya Corona vyapindukia 630
7 Februari 2020Uchunguzi kuhusu virusi vya corona umebainisha kuwa watu wengine 41 waliomo kwenye meli ya utalii kwa jina Diamond Princess, pia wameambukizwa virusi hivyo, na hivyo kufanya idadi jumla ya walioambukizwa ndani ya meli hiyo kufikia 61. Meli hiyo ambayo imewabeba takriban watu 3,700, imewekwa kwenye karantini kwa muda wa wiki mbili sasa tangu ilipowasili katika bandari ya Yokohama, kusini mwa Tokyo, baada ya abiria mmoja aliyeshuka kwenye meli hiyo kugunduliwa kuwa na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, watu 61 waliothibitishwa kuambukizwa ni miongoni mwa watu 272, ambao walipimwa kwa sababu walionyesha dalili za virusi hivyo au walikuwa karibu na abiria wa kwanza aliyeambukizwa.
Waziri wa Afya wa Japan Katsunobu Kato amewaambia waandishi wa habari kuwa watu 21 miongoni mwa 41 waliothibitishwa kuambukizwa ni raia wa Japan. Kato ameongeza kuwa uchunguzi zaidi utafanywa endapo abiria zaidi ndani ya meli hiyo wataonyesha dalili za kuugua.
Maafisa wa afya nchini Japan wameanza kuwaondoa wagonjwa kwenye meli hiyo kuwapeleka katika vituo vya afya.
Idadi ya vifo nchini China kutokana na mlipuko wa virusi hivyo kwa sasa imepindukia watu 630, akiwemo daktari Li Wenliang aliyetoa tahadhari ya mwanzo kuhusu kitisho cha virusi hivyo. Hadi sasa, upande wa China bara pekee zaidi ya watu 31,120 wameambukizwa.
Virusi hivyo vimesambaa pia katika zaidi ya mataifa 20 ambako visa 260 vimethibitishwa.
Wanasayansi Hong Kong wavumbua kifaa cha kupima virusi vya corona
Hayo yakijiri, wanasayansi katika chuo kikuu cha Hong Kong wa sayansi na teknolojia wamesema wamevumbua kifaa cha kupima na kugundua kwa haraka virusi hivyo kwa wanadamu.
Wakitangaza hatua hiyo, wanasayansi hao wamesema duniani kote, changamoto kubwa imekuwa kubaini kwa haraka uwepo wa virusi hivyo mwilini.
Timu hiyo imesema kifaa walichokivumbua kinaweza kubaini virusi hivyo kwa muda wa dakika 40 pekee, tofauti na mfumo unaotumiwa sasa unaotumia kati ya saa moja na nusu hadi saa tatu.
Wanasayansi kote duniani wanafanya juhudi kutafuta namna ya kutibu virusi hivyo vipya, ambavyo kwa sasa vinatishia kuwa janga la afya duniani.
Japan kuwazuia abiria wa meli kuingia
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ametangaza kuwa kuanzia Ijumaa, nchi yake haitawaruhusu abiria kutoka kwenye meli nyingine za utalii kuingia nchini humo, kama hatua ya kuepusha maambukizi zaidi nchini Japan.
Idara ya usafiri wa angani nchini Italia pia imesema kuwa safari za kutoka na kwenda China zitaendelea kufungwa kutokana na virusi vya Corona
Nayo serikali ya Ujerumani inataka kuwahamisha raia wake wengine walioko Wuhan China. Hayo ni kulingana na gazeti la Der Spiegel.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ujerumani iliwahamisha raia 100 pamoja na familia zao kutoka Wuhan.
Vyanzo: RTRE, APE