1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya COVID-19 Marekani vyapindukia 10,000

Daniel Gakuba
7 Aprili 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anaendelea kuwa katika chumba cha wagonjwa mahtuti, vifo vitokanavyo na COVID-19 nchini Marekani vyapindukia 10,000, Ujerumani kutumia app kufuatialia kuenea kwa virusi vya corona.

Coronavirus New York City USA
Picha: Reuters/B. McDermid

Habari za muda mfupi uliopita kutoka kwa msemaji wa serikali ya Uingereza, zimeeleza kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Boris Johnson anaendelea vyema katika chumba cha wagonjwa mahtuti, na ingawa hakuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua, alikuwa anaongezewa hewa ya oksijeni. Msemaji huyo, James Slack, hakutoa maelezo ya kina kuhusu namna hewa hiyo inavyosaidia katika matibabu ya Waziri Mkuu Johnson. 

Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye anaugua COVID-19Picha: picture-alliance/dpa/PA Wire/M. Dunham

Malkia wa Uingereza Elisabeth II amejiunga na orodha ya viongozi wengi wa dunia waliomtumia ujumbe wa pole Boris Johnson wakimtakia kupata nafuu haraka.

Marufuku ya mazoezi mchana mjini Paris

Katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris, mamlaka ya mji huo imepiga marufuku kufanya mazoezi nje kati ya saa nne asubuhi na saa moja jioni, baada ya wakazi wengi wa jiji hilo kumwagika mitaani mwishoni mwa juma kufurahia jua la majira ya machipuko, licha ya maelekezo ya kuepuka misongamano. Meya wa jiji hilo Anne Hidalgo amesema mazoezi yoyote mtaani yataruhusiwa tu wakati idadi ya watu katika mitaa hiyo itakapokuwa imepungua kabisa.

Mitaa ya jiji la Paris ikiwa mitupu kutokana na amri ya kutotoka njePicha: picture-alliance/Photoshot/Tang Ji

Hadi sasa wakazi wa mji huo walikuwa wakiruhusiwa muda wa saa moja wa kufanya mazoezi nje, huku wakibeba fomu zenye maelezo kwa maandishi kuhusu sababu yao ya kuwa nje.

Ujerumani yaigeukia TEHAMA

Hapa Ujerumani taasisi ya Robert Koch inayoratibu juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona imegeukia teknolojia ya mawasiliano ya kisasa kujaribu kuchunguza na kuelewa vyema zaidi namna virusi hivyo vinavyoenezwa. Imeunda App ya saa za kisasa iitwayo Corona Data Donation, maana yake, Mgao wa data za corona, ambayo watawaomba watu kujitolea kuiweka katika saa zao na aina nyingine ya vifaa vinavyovaliwa wakati wa kufanya mazoezi.

App hiyo itapima mpangilio wa usingizi na shughuli za kimwili miongoni mwa watumiaji, na itapeleka taarifa ambazo zitaiwezesha taasisi hiyo kuelewa mahali palipo na visa vingi vya virusi vya corona.

Katika taarifa nyingine kuhusiana na mripuko wa virusi vya corona, vifo vitokanavyo na virusi hivyo nchini Marekani vimepindukia 11,000, huku China, kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mripuko huu, haikuripoti tukio lolote la kifo.

Na huko Afrika, Senegal imemruhusu dikteta wa zamani nchini Chad Hissene Habre anayetumikia kifungo cha maisha, kwenda katika kifungo cha nyumbani kwa muda wa siku 60, kutokana na kitisho cha COVID-19. Hata hivyo, wizara ya sheria ya nchi hiyo imesisitiza kuwa Habre hakuachiwa huru.

ap, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW