Israel yaendeleza operesheni ya kijeshi Ukingo wa Magharibi.
4 Julai 2023Wanajeshi wa Israel wamesonga mbele na msako wa wapiganaji wa kipalestina kwenye kambi iliyopo katika Ukingo wa Magharibi. Ikiwa ni siku ya pili tangu msako huo uanze wapalestina 10 wameshauawa na maalfu wamekimbia na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa.
Wizara ya afya ya Palestina imesema 20 kati ya watu hao waliojeruhiwa wako katika hali mbaya. Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amelaani operesheni hiyo ambayo ameiita kuwa ni uhalifu mpya wa kivita.
Soma:Wahanga wa operesheni ya kijeshi ya Israel Jenin wafikia 10
Mamlaka ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi nan chi tatu za kiarabu zilizo na uhusiano na Israeli ambazo ni Jordan, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu na Jumuiya ya Nchi 57 za Ushirikiano wa Kiislamu zimelaani mashambulizi hayo ya Israel.
Mara baada ya operesheni kuanza utawala wa Palestina unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ulitangaza kusimamisha mawasiliano na Israel hatua iliyozua wasiwasi kwa Marekani na kwenye Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi wa Israel wanaendesha operesheni hiyo wakati ambapo waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu yuko chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa washirika wake wa kisiasa wa vyama vya mrengo mkali. Vyama hivyo vinamtaka Netanyahu achukue msimamo mkali kujibu mashambulio ya hivi karibuni yaliyofanywa dhidi ya walowezi wa kiyahudi, ikiwa pamoja na kuuliwa kwa walowezi wanne.
Soma:Israel yafanya operesheni kubwa ya kijeshi mjini Jenin
Moshi mzito ulionekana mara kwa mara juu ya kambi ya wakimbizi kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, mji ambao kwa muda mrefu umekuwa kambi muhimu ya wapiganaji wa kipalestina. Jeshi la Israel lilisema Jumatatu kuwa operesheni yake ni kwa ajili kulenga baadhi ya maeneo katika mji wa Jenin kwenye Ukingo wa Magharibi ikiwa ni sehemu ya juhudi zake kubwa za kukabiliana na ugaidi likiwemo eneo moja ndani ya kambi ya wakimbizi iliyo kando ya mji huo wa Jenin ambalo jeshi la Israel limesema lilikuwa linatumiwa na wapiganaji na wanamgambo.
Msemaji wa jeshi la Israel,admeli Daniel Hagari ameeleza kuwa Israel imeanzisha operesheni hiyo, kwa sababu mashambulio yapatayo 50 mnamo kipindi cha mwaka uliopita yalitokea kwenye mji wa Jenin.
Vyanzo:AP/DPA/RTRE/AFP