1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vyapindukia 40,000 Gaza

15 Agosti 2024

Wakati ambapo idadi ya vifo kutokana na vita vya Gaza ikipindukia watu 40,000, duru mpya ya mazungumzo ya kutaka kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas imefanyika nchini Qatar.

Wapalestina wakiomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao waliouawa huko Gaza
Wapalestina wakiomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao waliouawa huko GazaPicha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Vyanzo vya kuaminika kutoka kwa baadhi ya wanadiplomasia vimeripoti kuanza kwa mazungumzo hayo mjini Doha, ambapo wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar wamekutana na wajumbe wa Israel huku Hamas ikikataa kushiriki, lakini ikasema iko tayari kupokea taarifa ili kufahamu mambo yaliyojadiliwa.

Hamas wamesema hawahitaji mazungumzo mapya bali utekelezwaji wa makubaliano ya mpango uliopendekezwa na Marekani na wametupilia mbali masharti mapya ya Israel ya kutaka kuachiliwa kwa mateka 33 katika awamu ya kwanza ya makubaliano hayo.

Soma pia: Israel yaishambulia kwa mabomu Gaza licha ya ukosoaji wa vifo vya raia

Ikulu ya Marekani ya White House imezitolea wito pande zote kushiriki ili kufikia makubaliano na kusisitiza kwamba maendeleo zaidi bado yanawezekana katika siku zijazo. Mkuu wa idara ya ujasusi wa Marekani CIA, William Burns, Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani na mkuu wa idara ya ujasusi wa Misri Abbas Kamel ni miongoni mwa walioshiriki duru hii ya mazungumzo kama ilivyokuwa hapo awali.

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas,akilihutubia Bunge la Uturuki Picha: Adem Altan/AFP/Getty Images

Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wana matumaini kuwa duru hii ya mazungumzo ya kusitisha mapigano  inayoendelea huko Qatar huenda ikasaidia kuvimaliza vita hivyo. Abu Nidal Eweini ni mkazi wa Gaza.

"Ee Mola, tuna matumaini wataafikiana na kukomesha hali hii, kwa sababu watu wamechoshwa kabisa. Watu hawana nguvu tena, wamechoka mno."

Akizungumzia idadi ya vifo iliyopindukia watu 40,000 huko Gaza, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, amesema alipolihutubia Bunge la Uturuki mjini Ankara leo, kuwa atalitembelea eneo la Ukanda wa Gaza bila kujali iwapo hatua hiyo inaweza kuhatarisha maisha yake.

Umoja wa Mataifa wakosoa vitendo vya jeshi la ulinzi la Israel

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Haki za Binaadamu Volker TürkPicha: Kyodo News/IMAGO

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Haki za Binaadamu Volker Türk, amesema katika taarifa iliyotolewa mjini Geneva kwamba hali hii isiyoweza kufikirika imetokea kutokana na kushindwa mara kadhaa kwa Jeshi la Ulinzi la Israel kutekeleza kanuni za vita, na kwamba kiwango cha uharibifu uliofanywa na jeshi la Israel dhidi ya nyumba, hospitali, shule na majengo ya ibada ni cha kutisha mno.

Soma pia: Shambulio la Israel kwenye shule huko Gaza lalaaniwa kimataifa

Katika hatua nyingine, Msemaji wa White House anayeshughulikia masuala ya usalama wa taifa la Marekani, John Kirby, amesema taarifa zinaonyesha kuwa Iran haijaondoa uwezekano wa kuishambulia Israel, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuyatumia makundi ya wanamgambo inayoyafadhili. Kirby amesisitiza kuwa Marekani inafuatilia kwa karibu hali hiyo na iko tayari, ingawa ana matumaini kuwa hali haitofikia huko.

Wataalamu wa siasa za Mashariki ya Kati wanasema kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano huko Gaza huenda kunaweza kuishawishi Iran na washirika wake  kutolipiza kisasi dhidi ya Israel  kufuatia mauaji ya Kamanda wa Hezbollah Fuad Shukur na kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh, na hivyo kuepuka mzozo mpana zaidi wa kikanda.

(Vyanzo: AP,DPAE, AFP)