Vigogo wa soka Ulaya waondoka vichwa chini
27 Juni 2014Miongoni mwa miamba iliyoondolewa katika michuano hiyo ni mabingwa watetezi wa kombe la dunia, Uhispania, mabingwa wa dunia mara nne Italia, mabingwa wa mwaka 1966 Uingereza pamoja na Ureno.
Kuondolewa kwa miamba hiyo kumewafanya wachezaji nyota wa soka duniani kurejea nyumbani mapema kuliko vile ambayo walivyofikiria. Wachambuzi wa soka duniani wanasema wachezaji hao wakiongozwa na mchezaji bora wa dunia, Christiano Ronaldo pamoja na wengine wakiwemo Wayne Rooney, Xavi Hernandez na Adrea Pirlo wameondoka Brazil wakiwa na mikia katikati ya miguu yao kama ishara ya wakati mgumu zaidi waliokuwa nao katika michuano hiyo.
Licha ya idadi ya timu za ulaya zilizosonga mbele katika michuano hiyo kuwa ni sita sawa na michuano iliyopita ya kombe la dunia nchini Afrika kusini lakini hakuna ambaye alitegemea kuona vigogo vya soka katika bara hilo kama Ureno, Uhispania, Italia na Uingereza vikiondolewa mapema katika hatua ya makundi huku mataifa ya Marekani ya kaskazini na Kusini ambayo yalikuwa hayapewi nafasi kwa mfano, Costa Rica, Chile, Marekani na Mexico yakisonga mbele tena kwa kuonesha kandanda safi na la kuvutia.
Kocha mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps amesema kufanya vizuri kwa timu kutoka katika bara la Marekani kunatokana na kuyazoea mazingira ya bara hilo lakini pia uwepo wa mashabiki wao wengi viwanjani na mitaani.
"Tupo Brazil, kwa hiyo timu za Marekani zimezoea mazingira na labda pia kwasababu zinacheza karibu na nchi zao na uwepo wa mashabiki wengi ambao unawapa nguvu na ujasiri uwanjani" alisema Deschamps.
Nae mshambuliaji wa Brazil, Fred anaunga mkono kauli ya kocha huyo mkuu wa Ufaransa "nafikiri hali ya hewa inaweza ikachangia kuleta mabadiliko kidogo kwasababu tumeizoea lakini pia suala la ufundi nalo linaweza likaleta mabadiliko pia, tumeona Colombia, Ecuador, Uruguay, Chile zote zikicheza vizuri kutokana pia na kuzoea hali ya joto, inaweza ikawasaidia kidogo" alisema Fred
Kocha mkuu wa Uingereza, Roy Hodgson amesema timu za Ulaya zimeathiriwa na upinzani uliopo wa ligi zao za nyumbani. Roy ametoa mfano wa Costa Rica na Iran ambayo almanusuru itoke suluhu na Argentina kuwa zipo katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya vizuri katika michuano hiyo kutokana na kufanya maandalizi ya mapema hali ambayo inawafanya kuwa imara zaidi kiufundi.
"Iran na Costa Rica wamekua pamoja kwa miezi kadhaa hivyo wana nafasi kubwa ya kufanya kile ambacho sisi tungependa kukifanya kwa wiki tatu au nne" alisema Roy Hodgson.
Licha ya historia kuonesha kuwa hakuna timu yoyote kutoka bara la Ulaya iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la dunia katika bara la Marekani lakini mataifa hayo ya Ulaya yanajipa matumaini ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza huku ikizingatia kuwa katika fainali zilizopita nchini Afrika kusini matifa yote matatu ya ulaya yalimaliza katika nafasi za juu za michuano hiyo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman