Vijana na tamaduni za Kiafrika katika kukuza kilimo
12 Septemba 2025
Wataalam wanahoji kwamba ingawa kilimo kinawaajiri asilimia kubwa ya watu barani Afrika, kinachangia sehemu ndogo tu ya Pato la Taifa, jambo linaloonyesha haja ya ushirikishwaji bora zaidi wa vijana, hali inayotoa fursa kwa vijana kushiriki katika ujasiriamali na ubunifu kwenye sekta ya kilimo.
Kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa mataifa mengi barani Afrika, kikiwa kinachangia ajira, upatikanaji wa chakula na Pato la Taifa. Hata hivyo, sekta hii kwa muda mrefu imeonekana kama ya kizamani na isiyowavutia vijana. Wakati idadi ya vijana barani Afrika inakuwa kwa kasi kubwa, changamoto na nafasi katika kilimo zinajitokeza kwa nguvu mpya. Vijana wanaweza kuwa nguzo muhimu ya mageuzi ya kilimo iwapo watawezeshwa kupitia sera, ufadhili, mafunzo na teknolojia.
Mafunzo yaliyoandaliwa na Muungano wa Mashirika ya Kiraia yanayohusika na Chakula Bora na Salama barani Afrika, AFSA uliowaleta pamoja huko Gilgil, Nakuru, Kenya, vijana na wadau kwenye sekta ya kilimo kutoka mataifa 20. Mafunzo hayo yamejikita katika uzalishaji wa chakula salama kupitia pembejeo bora na asili kwa ajili ya bara la Afrika.
Nguvu kazi ya vijana katika kuboresha kilimo
Tabitha Munyiri, mshiriki kutoka Kenya anasema wanaangazia namna mataifa ya Afrika yanaweza kutumia nguvu kazi ya vijana kuboresha kilimo. ''Tunaangalia jinsi tunavyoweza kujenga uwezo wa vijana wetu ambao wako kwenye mstari wa mbele kutetea na kuhimiza uhuru wa kutumia mbinu za kilimo na pembejeo zinazoweza kuwapa chakula kwa wingi,'' alisema Tabitha.
Licha ya nafasi kubwa iliyopo, vijana hukumbana na changamoto nyingi zinazowazuia kuingia au kustawi katika kilimo. Kwanza ni mtazamo hasi kuhusu kilimo kwani vijana wengi hudhani kilimo ni kazi ya sulubu, iliyopitwa na wakati na isiyo na faida. Upungufu wa elimu ya kilimo cha kisasa, utafiti na mbinu bunifu huwafanya kukosa mvuto wa kujiingiza kwenye kilimo.
Ukosefu wa teknolojia na mafunzo pia huwaathiri hasa wanapojiingiza kwenye kilimo bila mafunzo ya jinsi wanavyoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame, mafuriko na magonjwa ya mimea yanayohatarisha kipato kutokana na kilimo.
Baadhi ya wanaojitosa kwenye kilimo hukabiliwa na upungufu wa mitaji na mikopo kwani benki nyingi na taasisi za kifedha hazitoi mikopo kwa urahisi kwa vijana kutokana na ukosefu wa dhamana na rekodi za kifedha. Upungufu wa ardhi ni changamoto nyingine, kwenye jamii nyingi, ardhi inamilikiwa na wazee au ukoo, jambo linalowafanya vijana washindwe kupata ardhi ya kuendeleza kilimo cha kisasa.
Wataalam wa kilimo wanasema vijana ni nyenzo muhimu kwa mageuzi ya kilimo barani Afrika. Mtaalamu wa kilimo Hawa Gaye anasema changamoto walizo nazo zinaweza kushughulikiwa kupitia ushirikiano wa mataifa, uwezeshaji wa sera na teknolojia, pamoja na ufadhili wa miradi bunifu.
''Hatua ya kujumuishwa vijana katika masuala haya ya ikolojia ya kilimo ni muhimu sana kwa sababu litahakikisha uendelevu na pia mwendelezo wa kazi kubwa tunayofanya kuyalinda mazingira yetu, kuilinda sekta yetu ya mbegu na pia kuilinda mifumo yetu ya chakula,'' alifafanua Hawa.
Serikali za Afrika zimechukua hatua kadhaa
Ili kutambua nafasi ya vijana katika kilimo, serikali za Afrika pamoja na mashirika ya kikanda na ya kimataifa yamechukua hatua kadhaa. Ajenda ya mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika inalenga kuifikia Afrika yenye usalama wa chakula na uchumi wa viwanda, ambapo vijana wanachukuliwa kama injini kuu ya mabadiliko ya kilimo.
Mpango wa Ushirikiano Mpya kwa Maendeleo ya Afrika, NEPAD, ambao ni wa maendeleo ya kiuchumi wa Umoja wa Afrika, unaweka lengo la takribani asilimia 10 ya bajeti ya kitaifa kutengwa kwa kilimo ili kuongeza uwekezaji, ikiwemo uwezeshaji wa vijana. Mashirika ya kimataifa kama Shirika la Kilimo Ulimwenguni, FAO na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD, yamezindua miradi ya kuendeleza kilimo cha vijana kupitia mikopo midogo, mafunzo ya ujasiriamali na upatikanaji wa teknolojia.
Aidha, Hawa anasema programu za jumuiya za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Pembe ya Afrika, IGAD, Jumuia ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC zinashirikiana kusukuma ajenda za uwezeshaji wa vijana katika kilimo, hasa kupitia mafunzo ya kitaaluma, upatikanaji wa masoko ya kikanda na miradi ya pamoja ya kilimo.
''Tunawahitaji pia watunga sera wetu na tunatoa wito kwa Umoja wa Afrika kuangalia kwa karibu mipango iliyowekwa na pia kanuni hizi na mifumo hii wanayoileta Afrika,'' alibainisha Hawa.
Mikakati ya kitaifa kwenye nchi kama Kenya, Nigeria na Rwanda zimeanzisha mipango maalum ambayo inalenga kuwashawishi vijana kuingia kwenye kilimo cha kibiashara. Wataalam wanahimiza kilimo kinachozingatia mazingira kupitia mbinu za kilimo zinazochanganya mbinu za jadi na za kisasa.
Utamaduni na mila za Kiafrika zinashikilia mifumo tajiri yenye maarifa ambayo vijana wanaweza kutumia kufanya kilimo cha kisasa na kuendeleza kilimo, huku wakiendelea kujikita katika utambulisho na urithi. Mbinu za jadi za kilimo kama vile mzunguko wa mazao, kilimo mseto, na udhibiti wa wadudu wanaosababishwa na athari za matumizi ya mbegu za kisasa za GMO, na utoaji wa hewa chafu ya kaboni, zimetumika kwa karne nyingi.
Jinsi utamaduni na mila zinavyoweza kutumika katika kilimo
Vijana wanaweza kufanya mazoea haya kuwa ya kisasa kwa kuyachanganya na uvumbuzi wa kisayansi. Daniel Wanjama, mratibu katika kampuni ya Seed Savers Network, shirika linalohimiza matumizi ya mbegu za kiasili anasema uhuru huanza na wao wenyewe kujivunia kama watu. Kulingana na Wanjama, wana washirika ambao wanatoa hamasa kuhusu jinsi ya kuheshimu utamaduni wao na mila zao na jinsi wanavyoweza kutumia utamaduni na mila katika kilimo.
Utamaduni na mila za Kiafrika huwapa vijana sio tu ujuzi wa kilimo, lakini pia utambulisho, hadhi, na ari ya kuungana pamoja ambayo inaweza kukifanya kilimo kuwa endelevu zaidi, kuwa na ubunifu, na chenye kuvutia. Kwa kuchanganya mbinu za kilimo za kitamaduni na kisasa, vijana wanaweza kugeuza kilimo kuwa fursa ya kiuchumi na urithi wa Kiafrika.
Pamekuwa na miito mingi ya kuwahamasisha vijana kujihisisha na kilimo. Bila shaka vijana wamehamasika vya kutosha katika kuchangamkia fursa kwa vijana kushiriki katika ujasiriamali na ubunifu kwenye sekta ya kilimo barani Afrika.