1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wa Tunisia hawautaki Uislamu wa siasa kali

9 Agosti 2011

Kufuatia Mapinduzi ya Yasmini, Waislamu nchini Tunisia wamepata umaarufu mpya. Rasmi wanapinga kuhusishwa na Al-Qaeda. Hata hivyo wanazusha wasiwasi.

Nur für das Projekt 9/11: Spurensuche Tunesien

Baada ya Mapinduzi ya Asumini, kama vile yalivyoitwa na vyombo vya habari, ambapo vuguvugu la umma lilimn'gowa madarakani Rais Zine al-Abidine Ben Ali wa Tunisia mapema mwaka 2011, mbali ya harakati za kisiasa za kiliberali na zile za sera za mrengo wa shoto, Waislamu wa itikadi kali wameibuka tena katika ulingo wa kisiasa nchini Tunisia. Chini ya utawala uliopita wa Ben Ali, harakati zao zilipigwa marafuku na kukandamizwa moja kwa moja. Waislamu hao wa itikadi kali wa Tunisia wanajitenganisha kwa makusudi na itikadi ya matumizi ya nguvu ya kundi la Al Qaeda. Lakini matlaba yao yanagongana na tabaka la vijana wasomi kwenye viunga vya miji na, kwa vyovyote vile, hawaaminiwi.

Mazungumzo kuhusu siasa pia katika mtaa wa Habib BourguibaPicha: DW

Mojawapo ya mandhari inayokutikana katika mtaa wa Habib Bourgiba mjini Tunis ni mjalada wa kisiasa kati ya kundi dogo la wanaume wenye madevu waliovalia kanzu zilizo pana. Katika mjadala huo, kuna wanaoona suala la kutenganisha dini na dola ni sawa na kumkufuru Mungu, wakati mchangiaji mmoja anakaripia kile alichokiita "jamii iliyoharibika".

Hofu ya vijana wa kimapinduzi

Tukio la mapinduzi ya Tunisia miezi kadhaa iliyopita lilikuwa halifikiriki kabisa. Sio mbali na eneo la matembezi, Cyreen Belhedi anakutana na marafiki zake kwenye mojawapo ya mikahawa mingi iliyoko katika mtaa wenye harakati nyingi mjini Tunis. Vijana wa kike na wa kiume wakiwa katika kiwewe cha furaha wanavuta sigara, wanakunywa kahawa, chai na juisi na wengine wanabwia hata pombe. Vijana hao wanawaangalia wanaume wenye ndevu refu walioko karibu na hapo kwa jicho la kutowaamini.

Maisha ya Kawaida katika mtaa wa Habib BourguibaPicha: DW

Cyreen, mwanamke mwenye umri wa miaka 27, anasema kuwa watu hao walimtia hofu wakati wa mapinduzi ya Tunisia ya vuguvugu la umma, ambayo alishiriki kikamilifu kwa kuingia barabarani kila siku kujiunga na waandamanaji. "Mara nyengine nikiwa mkahawani au kwenye kilabu ya pombe, hufikiria kwamba watakuja kututwanga risasi au kuturipua kwa mabomu. Ni kweli kwa hivi sasa hawajishughulishi na mambo mengi, lakini wanataka tu kuitumia hali hiyo kujijenga imara." Anasema Cyreen.

Hata wanaharakati wa Kiislamu wa Tunisia waikana Al-Qaida

Kundi lililo mashuhuri kabisa la Waislamu wa itikadi kali nchini Tunisia, ni chama cha Ennahda, ambacho kilikuwa kimepigwa marufuku kwa muda mrefu. Chama hicho kimeingia tena katika ulingo wa kisiasa nchini humo.

Kiongozi wa chama cha Nahda, Rachid Al-GhannouchiPicha: DW

Rashid Al- Ghannoushi, mwenye umri wa miaka 70, ni mcha Mungu na kiongozi wa chama hicho. Daima kunakuwa na mlinzi kwenye mlango wa nyumba yake, na wakati alipokutana na watu waliomtembelea nyumbani kwake kutaka kujuwa kuhusu habari za kuogopwa kwa chama chake, Al- Ghannoushi aliwahakikisha kwamba kuhofiwa kwa chama chake ni jambo lisilokuwa na haki kabisa. "Hofu hizo zimekuwa zikiendelea chini ya msingi wa biashara ya hofu iliyokuwa ikiendeshwa na rais wa zamani Ben Ali kwa kuwazima wapinzani wake wa kisiasa. Lengo la chama chetu ni kulinda umoja wa wananchi, kusafisha jamii kutokana na mabaki ya utawala wa Ben Ali na kuendeleza ujenzi wa demokrasia huru ya kiraia itakayowashughulikia wananchi wote kwa kuzigatia usawa." Anasema Al- Ghannoushi.

Ameendelea kusema kwamba kwa kitu kama hicho hakuna haja ya mtu kuogopa. Kuhusu al-Qaida na sera yake ya matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzani wao, Al- Ghannoushi anajitenga kabisa na itikadi hizo za mtandao huo unaohusishwa na mashambulizi ya tarehe 11 Dseptemba 2001. "Sisi siku zote tumekuwa tukisema na tunasena tena leo hii kwamba harakati za al-Qaida sio halali huo ni ugaidi." Anasema Al- Ghannoushi.

Bado kazi ya mageuzi haijakamilika

Tatizo moja: Kupambana na rushwaPicha: DW

Hata chama cha Tahrir, ambacho ni chama chengine kinachofuata itikadi kali za Kiislamu, kinajitenga mbali na ugaidi, ingawa kinasema wazi kwamba kinataka kuwepo kwa dola ya Kiislamu nchini Tunisia. Msemaji wake, Bel-Haj, mwanamme wa umbo fupi la kuvutia, alifikia umbali wa hata kukubali kufanya mahojiano kwenye mkahawa mmoja katika mtaa wa Bourguiba.

Bel-Haj anaona kuwa uasi wa umma nchini Tunisia na Misri bado haujamalizika. Anasema hatua ya pili ni kwa Waislamu duniani kote watambuwe kwamba inabidi wajisimamie wenyewe. Watadai kuanzishwa kwa taifa la Kiislamu ambapo kwayo raia watatekeleza Uislamu kwa vitendo. Amemalizia kwa kusema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika hilo, na wakati wananchi watakapokuwa na utambuzi wa kiroho wa Uislamu, hapo yanaweza kufanikishwa hata yale yasiowezekana.

Vipi ikiwa Tunisia itaongozwa Kiislamu?

Kuandamana ili kupigania uhuruPicha: DW

Kwenye mkahawa mwengine, hali ya uchangamfu imeendelea kutanda, Cyreen na marafiki zake wanafurahia maisha. Wanasema hawawezi kufikiria kama kuna siku Tunisia itakuja kuongozwa na Waislamu wa itikadi kali. Lakini kwa kiasi gani wana uhakika kwamba jambo hilo halitatokea? Iwapo hilo litatokea, Cyreen anasema yeye na marafiki zake wataihama nchi hiyo, kwani mapinduzi yao yatakuwa hayana maana.

Mwandishi: Khalid Khaoutit/ZPR

Tafsiri: Mohamed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW