Vikosi vya Burkina Faso vyawaokoa mateka
16 Januari 2016Kabla ya shambulio hilo la Ijumaa nchi hiyo ilikuwa haikuguswa na mashambulizi ya aina hiyo kutoka makundi ya wapiganaji wa jihadi kusini mwa jangwa la Sahara ambayo yamekuwa yakiwakumba nchi jirani zao.
Shambulio hilo linakuja kufuatia shambulio kama hilo hapo mwezi wa Novemba katika hoteli moja ya kifahari kwenye mji mkuu wa Mali Bamako ambalo limeuwa watu 20 wakiwemo raia wa Urusi,China na Marekani.
Shambulio hilo katika mji mkuu wa Ouagadougou linalodaiwa kufanywa na kundi la AQIM ambalo ni tawi la Al Qaeda katika eneo la Maghreb barani Afrika linaashiria kutanuka kwa operesheni za wanamgambo wa itikadi kali ambayo yamekuwa yakiungana upya na kuimarisha harakati zao wakifuata nyazo za kundi la Dola la Kiislamu huko Mashariki ya Kati.
Waburkinabe watakiwa kuwa macho
Rais Roch Marc Christian Kabore wa Burkina Faso akilitembelea eneo la shambulio hilo amekaririwa akisema " Hali tunayoipitia nchini Burkina Faso haina kifani.Hivi ni vitendo vya kuchukiza na woga na wahanga ni watu wasiokuwa na hatia."
Amewataka wananchi wa Burkinabe wawe macho kwamba lazima wavijumuishe vitendo hivyo vya kigaidi kama sehemu ya mapambano yao ya kila siku.
Kabore amesema watu 23 kutoka nchi 18 tafauti wameuwawa katika shambulio hilo kwenye Hoteli ya Spelndid na kilabu cha kamari kilioko karibu ambavyo ni mashuhuri kwa wananchi wa mataifa ya magharibi na wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini humo.
Maafa na majeruhi
Serikali haikutowa maelezo zaidi kuhusu wahanga hao.Balozi wa Ufaransa nchini humo Gilles Thibault amesema katika mtandao wake wa Titter kwamba idadi ya watu waliouwawa ni 27 na mateka kama 120 wameachiliwa huru wakati wa operesheni iliyosaidiwa na wanajeshi wa Marekani na Ufaransa.
Maafisa wa serikali ya Burkinabe wamesema takriban watu 33 wamejeruhiwa na kwamba washambuliaji wanne akiwemo Mwarabu mmoja na Waafrika weusi watatu wameuwawa.
Wakati huo huo imefahamika kwamba daktari mmoja wa Austria na mkewe wametekwa nyara wakati wa usiku kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Mali.Utekaji nyara huo umetokea katika eneo la Baraboule na bado haiko wazi iwapo tukio hilo linahusina na shambulio la hoteli.
Walengwa wa shambulio
Shambulio dhidi ya hoteli hio lilianza Ijumaa saa mbili na nusu usiku wakati kawaida eneo hilo huwa limejaa watu. Washambuliaji waliyatia moto magari na kufyatuwa risasi hewani kuwarudisha watu nyuma kutoka kwenye jengo hilo kabla ya kuingia ndani ya hoteli na kuwashikilia watu mateka.
Daktari mmoja aliyewatibu baadhi ya majeruhi wa shambulio hilo amesema walimwambia kwamba washambuliaji walionekana kuwalenga raia wa mataifa ya magharibi katika shambulo lao hilo.
Shughuli za kuikombowa hoteli hiyo ya vyumba 147 zilikuwa za pole pole kutokana na mabomu yaliyotegwa na wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu.
Mandishi : Mohamed Dahman / Reuters
Mhariri : Yusra Buwayhid