1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Haftar vyaishambulia Tripoli

Admin.WagnerD14 Aprili 2020

Vikosi vya mbabe wa kivita nchini Libya Khalifa Haftaleo nvimeushambulia kwa maroketi mji mkuu, Tripoli baada ya kupoteza miji muhimu upande wa magharibi iliyokamatwa na wapiganaji tiifu wa upande wa serikali.

Libyen Symbolbild LNA
Picha: Reuters/Esam Omran Al-Fetori

Duru zimearifu kuwa vikosi vya Haftar vimevurumisha mfululizo wa maroketi yaliyosababisha miripuko mikubwa usiku kucha mjini Tripoli ikizilenga nyumba kadhaa karibu na kambi ya jeshi ya Mitiga iliyopo mashariki ya mji huo.

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema sehemu kubwa ya mashambulizi yamelenga makaazi ya raia kwenye kitongoji cha Tajoura huku moja ya roketi liliishambulia gari ya wagonjwa karibu na mji wa Misrata na kumuua mfankazi mmoja wa afya.

Serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ambayo kwa karibu mwaka mmoja inapambana kubakia na udhibiti wa mji mkuu, Tripoli, imevituhumu vikosi vya Haftar kulipa kisasi kwa kuwashambulia raia baada ya kupoteza maeneo muhimu siku ya Jumatatu.

Msemaji wa serikali hiyo Mohamad Gnounou amesema wapiganaji wenye silaha wamefanya mashambulizi mjini Tripoli bila kubagua na kuelekeza hasira zao kwa wakaazi wa mji huo.

Upande wa Haftar wapata pigo 

Wapiganaji wa upande wa serikali ya LibyaPicha: picture-alliance/Photoshot/H. Turkia

Siku ya Jumatatu serikali hiyo iliikamata miji miwili ya pwani ya Sabratha na Sorman pamoja na maeneo mengine kadhaa kutoka mikononi mwa vikosi vya Haftar.

Kulingana na serikali mjini Tripoli miji hiyo miwili ilikamatwa baada ya saa sita za mapigano makali ya ardhini na msaada wa ndege za kivita.

Sorman na Sabratha inakutikana kiasi kilometa 70 magharibi ya Tripoli karibu na mpaka na Tunisia na kukombolewa kwake ni pigo kubwa kwa vikosi vya Haftar.

Katika ukasara wake wa Facebook vikosi vya upande wa serikali vilichapisha picha za mitambo ya kufyetua maroketi , vifaru 10 vya jeshi na magari mengine ya silaha nzito waliyosema wameyakmata katika miji hiyo ilikuwa chini ya udhibiti wa wapiganaji wa kisalafi wanaomtii Haftar.

Kwa karibu muongo mzima Libya imetumbukia kwenye machafuko tangu kuondolewa madarakani kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghadafi wakati wa maandamano ya umma mwaka 2011.

Mamia ya watu wamekufa na wengine kukimbia makaazi yao 

Mbabe wa kivita, Khalifa HaftarPicha: picture-alliance/ Balkis Press

Umoja wa Mataifa umesema tangu vikosi vya Haftar vilipoanzisha mashambulizi ya kuumata mji mkuu Tripoli mami ya watu wamekufa na   zaidi ya wengine 200,000 wameyahama makaazi yao.

Katika wiki chache zilizopita kiasi watu 3,700 wameyakimbia maskani yao katika wilaya ya Abusleim mjini Tripoli.

Kadhalika zaidi ya watu milioni mbili ikiwemo watoto laki 6 wanaoishi mjini Tripoli wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na ukosefu wa umeme kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu muhimu.

Mratibu wa msaada wa kuutu wa Umoja wa Mataifa kwa Libya ameonya dhidi ya pande hasimu kutumia huduma muhimu kama silaha ya kivita hasa wakati ambapo Libya inakabiliana na kusambaa virusi vya corona.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Iddi Ssessanga