Vikosi vya Haftar vyalipuuza pendekezo la GNA
24 Agosti 2020Msemaji wa vikosi vya Haftar, Ahmed al-Mosmari ameuambia mkutano wa waandishi habari uliofanyika kwa njia ya televisheni kwamba pendekezo hilo linaundanganya umma wa Libya pamoja na jumuiya ya kimataifa na kuliita la 'udanganyifu', akidai kuwa wanamgambo pinzani walikuwa wanajiandaa kuushambulia mji wa kimkakati wa Sirte.
Amesema mpango huo una dhamira ya kuficha ukweli kuhusu nia yao nchini Libya, akizitolea mfano Uturuki na Qatar, wafadhili wakuu wa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kwenye mji mkuu, Tripoli.
Abdullah Blaihek, msemaji wa baraza la wawakilishi ambalo lina makao yake mashariki mwa Libya ambalo linaungwa mkono na Haftar amekaribisha juhudi hizo za kusitisha mapigano.
''Mzozo wa kisiasa wa Libya lazima umalizwe kwanza kwa kuunga mkono usitishaji mapigano, kisha kuwafukuza mamluki wa kigeni ambao wameletwa Libya na pia kuanzisha tena uuzaji wa mafuta, kwa sharti kwamba hili linafanyika kwa haki na uwazi katika masuala ya mapato yatokanayo na mafuta,'' alisisitiza Blaihek.
Siku ya Ijumaa, Fayez Sarraj, mkuu wa serikali ya Tripoli alitangaza kusitisha mapigano na kutoa wito wa kuviondoa vikosi vya kijeshi kwenye mji wa Sirte na eneo la karibu la Jufra, hatua inayomaanisha kuondolewa kwa vikosi vya Haftar.
Pendekezo hilo lililotolewa baada ya shinikizo la jumuia ya kimataifa, linaonekana kama mafanikio, huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa vita vipya vinavyochochewa na mataifa yenye nguvu, wakati ambapo pande zinazohasimiana zikijiandaa kwa vita huko Sirte.
Maandamano yatawanywa kwa milio ya risasi
Hayo yanajiri wakati ambapo watu wenye silaha walifyatua risasi hewani kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wanaandamana jana kupinga hali ngumu ya maisha kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli pamoja na kuipinga serikali.
Waandamanaji walikusanyika kwenye makao makuu ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ya mjini Tripoli, GNA kuelezea hasira yao kutokana na kile walichokiita "kifo cha taratibu" kutokana na kudhoofika kwa huduma za umma, rushwa na hali ngumu ya uchumi.
Baada ya hapo walielekea kwenye mnara wa kumbukumbu wa mashujaa ulioko katikati mwa Tripoli, ambako watu wasiojulikana waliwatawanya kwa kufyatua risasi za bunduki na kusababisha hali ya wasiwasi mkubwa. Wizara ya mambo ya ndani ya Libya imesema mtu mmoja alijeruhiwa na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, limesema kuwa Shirika la Hilali Nyekundu la Libya, limeiopoa miili ya wahamiaji 22 katika pwani ya mji wa Zwara hapo jana.
Soma zaidi:Pande zinazohasimiana Libya zatoa wito wa kusitisha mapigano
Mkuu wa IOM nchini Libya, Federico Soda amesema kwamba watu 37 walionusurika baada ya kuokolewa na wavuvi wamesema takriban watu wengine 45 wakiwemo watoto watano wamekufa baada ya injini ya boti waliyokuwa wakisafiria kulipuka katika pwani ya Zwara.
(AP, AFP, Reuters)