Vikosi vya Iraq vyapenyeza zaidi mji wa Mosul
4 Novemba 2016Kamanda wa kitengo maalum cha kukabiliana na ugaidi anayeongoza mashambulizi hayo amesema vikosi vyake vimefanikiwa kuzingira eneo kubwa waliko wapiganaji hao wa IS.Vikosi hivyo vya Iraq vimechukua udhibiti wa eneo la Malayeen, Samah, Khadra,Karkukli,Quds na Karama katika mashambulizi yaliyosababisha hasara kubwa kwa wapiganaji wa IS.Vikosi hivyo kisha viweka Bendera ya Iraq katika majengo yaliyokuwa yakisimamiwa awali na wapiganaji hao.Sehemu iliyotekwa na vikosi vya serikali ni kipande tu cha mji huo wa Mosul ambao umegawanywa maeneo ya makaazi na viwanda.Mji huo ambao umekuwa chini ya usimamizi wa IS tangu mwaka 2014 una wakaazi millioni 2.
Operesheni hiyo ya kuwatimua wapiganaji hao kutoka mji wa Mosul ndio kubwa zaidi ya ardhini kuwahi kufanyika nchini Iraq tangu ile iliyoongozwa na Marekani mwaka 2003,na huenda ikaamua hatma ya wapiganaji hao wa IS ambao wamekaidi ulimwengu kwa kipindi cha miaka miwili. Shirika la Umoja wa mataifa limesema wakati operesheni hiyo ikiendelea wapiganaji hao wameendelea kuwaua mamia ya watu ikiwa ni pamoja na wasiotaka kujiunga nao na wafanyikazi wa zamani 180 wa serikali ya Iraq.Kundi hilo pia limehusishwa na utekaji kwa mujibu wa Ravina Shamdasani ambae ni msemaji wa ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu katika shirika hilo la Umoja wa mataifa "Tuna taarifa kuwa wanamgambo wa IS wanawazulia mateka karibu akinamama 400 wa Kikurdi,Yazidi au wale wa Kishia huko Tal Afar. Tangu Octoba 17 kundi hilo la IS limeripotiwa kuwasajili kwa nguvu watoto walio umri wa miaka 9 au 10 kama wapiganaji katika mji wa Mosul."
Kufikia sasa maeneo yaliyotekwa na vikosi vya Iraq kutoka kwa IS hayana watu wengi kama maeneo mengine,hasa ukanda wa magharibi wa mto Tigris ambao idadi kubwa ya watu wake ni Waisamu wa Kisunni na huenda pia wamekita mizizi Wasunni wenye msimamo mkali .Vikosi vya Iraq na vile vya Marekani vinavyoendesha operesheni ya angani na ardhini vimesema vimefanikiwa kuindesha kwa haraka kuliko ilivyotazamiwa ,lakini vikashikilia bado operesheni hiyo imo katika hatua za kwanza.Shirika la Umoja wa mataifa limesema watu elfu 22 wametoroka makwao tangu kuanza kampeini hiyo ya kuukomboa mji wa Mosul,bila kuhesabu maelfu ya wengine kutoka ijiji jirani vya na mji huo waliolazimishwa kwenda Mosul na wapiganaji wa IS ili kuwatumia kama ngao.
Mwandishi:Jane Nyingi/RTRE/APE
Mhariri:Yusuf Saumu