1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Israel bado vyaushambulia mji wa Rafah

13 Juni 2024

Marekani yasema Israel inaunga mkono makubaliano ya usitishaji vita wakati Hamas wakitaka yafanyike kwanza marekebisho kwenye mpango uliopendekezwa.

Waziri wa ulinzi wa Israel Joav Gallant
Waziri wa ulinzi wa Israel Joav Gallant akiwa RafahPicha: Ariel Hermoni/Israel Mod/IMAGO

Vifaru vya kivita vya Israel vimeendelea kusogea zaidi katika maeneo ya Magharibi mwa mji wa Rafah huko Gaza, katika moja ya mashambulio mabaya zaidi kushuhudiwa kwenye eneo hilo.

Wakaazi wa maeneo hayo wamesema Israel imeshambulia kutoka angani, ardhini na baharini na familia nyingi kulazimika kukimbia makaazi yao usiku.

Wakaazi wa Rafah wamesimulia hali ilivyo,wakisema wanajeshi wa Israel walivamia wakielekea eneo la Al-Mawasi ambalo liko karibu na ufukwe ambao kimsingi umetengwa na Israel yenyewe kama sehemu ya shughuli za  kutowa huduma za kibinadamu, kama ilivyotangaza na kuchapisha pia kwenye ramani tangu lilipoanzisha operesheni ya Rafah mwezi Mei.

Kwenye taarifa yake,lakini jeshi hilo la Israel limekanusha kwamba limefanya mashambulio yoyote ndani ya eneo hilo la Al Mawasi.

Badala yake Israel imesema mashambulio yake yanalenga kuangamiza vikosi vya  mwisho vya wanamgambo wa Hamas vilivyoko Rafah,mji ambao kabla ya mashambulizi haya ya sasa ulikuwa makaazi ya zaidi ya watu milioni moja.

Wapalestina waliokimbia mashambulizi RafahPicha: Doaa Albaz/Anadolu/picture alliance

Operesheni za kuwalenga Hamas ?

Wengi wa watu hao sasa wamekimbilia Kaskazini kuelekea miji ya Khan Yunis na Deir Al Balah,katikati ya Ukanda wa Gaza.

Jeshi hilo la Israel kwenye taarifa yake limesema  kwamba linafanya kile lilichokiita operesheni za kuwalenga Hamas kwa kuzingatiwa taarifa za kiintelijensia, katika mji wa Rafah na kupitia operesheni hizo, tayari wamegunduwa silaha na kuuwa Wapalestina waliokuwa na silaha.

Maeneo 45 yalilengwa na jeshi hilo katika Ukanda wa Gaza kupitia mashambulio ya anga,ikiwemo majengo ya shughuli za kijeshi,maeneo ya wanamgambo,na njia za chini kwa chini.

Mpaka sasa Israel imeondowa uwezekano wa kufikia makubaliano ya amani hadi watakapoliangamiza kabisa kundi la wanamgambo la Hamas, lakini kundi hilo inaonesha bado linapambana huku wanamgambo wakijitokeza upya kupambana katika maeneo ambako tayari wanajeshi wa Israel walishatangaza kuyasafisha.

Wanajeshi wa Israel karibu na RafahPicha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Juhudi za kiplomasia zaendelea 

Kufikia wakati huu wajumbe wanaosimamia juhudi za kutafuta makubaliano ya usitishaji vita hivyo kutoka Qatar,Marekani na Misri wanasema bado zinaendelea.

Jana  Alhamisi Mshauri wa Ikulu ya White House wa masuala ya kiusalama ya Marekani Jake Sullivan, alisema Israel inaunga mkono makubaliano ya kusitisha vita, yaliyopendekezwa na lengo hivi sasa ni kuziba mianya iliyopo upande wa kundi la Hamas na hatimae makubaliano yapatikane hivi karibuni.Soma Pia-Blinken: Tumedhamiria kusitisha vita Ukanda wa Gaza

Kundi hilo liliridhia makubaliano hayo mapya yaliyopendekezwa na Marekani lakini likataka yafanyike marekebisho kadhaa,likitilia mkazo msimamo wake kwamba makubaliano ya aina yoyote yatapaswa kuweka wazi suala la kumalizika kabisa kwa vita,jambo ambalo bado Israel inalipinga.

Kwa maana hiyo kwa mujibu wa Marekani hivi sasa mpira uko kwa Hamas.

Na hilo linatokana na kauli aliyoitowa Sullivan jana akizungumza  na waandishi habari  pembezoni mwa mkutano wa kundi la nchi tajiri kiviwanda G7huko Kusini mwa Italia.

Alisema ulimwengu unapaswa kulihimiza kundi la Wanamgambo wakipalestina kukubali pendekezo lililopo na kuepusha mkwamo.