1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia Kaskazini mwa Allepo

Angela Mdungu
28 Machi 2019

Syria imesema vikosi vya Israeli vimefanya mashambulizi Kaskazini mwa mji wa Aleppo siku ya jumatano na vikosi vya Syria vimejibu kwa kudungua makombora kadhaa

Aleppo: Symbolbild Israelischer Anschlag
Picha: picture-alliance/dpa/S. Kremer

Shambulizi hili ni la kwanza kufanywa na Israel ndani ya Syria tangu Rais wa Marekani Donald Trump aliposaini ilani ya kuitambua milima ya Golani kuwa sehemu ya Israel.

Shirika la habari la Syria SANA limesema vikosi vya anga vya nchi hiyo vimejibu mashambulizi  ya Israel yaliyolenga maeneo kadhaa ya viwanda ya Sheikh Najjar, Kaskazini Mashariki mwa Aleppo. Shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria limesema, Israel imeshambulia ghala la kuhifadhi silaha ambalo ni mali ya vikosi vya Iran na makundi washirika hivyo kusababisha mlipuko mkubwa uliouwa watu wanne wanaoaminika kuwa  walinzi wa ghala hilo. Hadi sasa Israel haijatoa maelezo yoyote juu ya madai ya kuhusika kuishambulia Syria.

Giza latanda baada ya Mashambulizi

Baadhi ya wakazi wa Alepo wameliambia shirika la habari la AFP kwamba, shambulizi hilo limesababisha umeme kukatika kwenye mji wote ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo ukiwa ni kituo kikubwa cha viwanda.

Vikosi vya Syria mjini AleppoPicha: Reuters/R. Said

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewahi kunukuliwa akisema nchi yake imefanya mamia ya mashambulizi  ya anga nchini Syria katika miaka michache iliyopita wakilenga sehemu zinazoshikiliwa na hasimu mkubwa Iran pamoja na washirika wake, wanamgambo wa Hezbollah kutoka Lebanon. Lengo la mashambulizi hayo linatajwa kwamba ni kuizuia Iran kujiingiza kijeshi nchini Syria.

Iran ni mshirika mkubwa wa Rais Bashar Al Assad kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Mwezi Januari mwaka huu Israel ilishambulia mitambo kadhaa ya Iran ndani ya Syria, saa chache baada ya kuliangusha kombora lililorushwa kutoka upande wa Syria. Kulingana na shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria, watu 21 waliuawa katika mashambulizi hayo, wengi wao wakiwa raia wa Iran.

Mwandishi :Angela Mdungu/AFPE/RTR

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW