Vikosi vya Kenya vyawaandama Al Shabab kusini mwa Somalia
18 Oktoba 2011Tangu serikali ya Kenya mjini Nairobi ilipothibitisha Jumapili iliyopita, imetuma wanajeshi wake Somalia kupambana na wanamgambo wa Al Shabab wanaotwikwa jukumu la visa vya kutekwa nyara watu nchini humo, jeshi la Kenya limesema limeingia umbali wa kilomita 120 ndani nchini Somalia, likisaidiwa na jeshi la anga.
"Wanajeshi wetu watalenga opereshini zao katika eneo la Afmadow, wameshaanza kuingia tangu Jumatatu usiku" amesema msemaji wa jeshi, kamanda Emmanuel Chirchir wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari na kuongeza "tunanukuu, "Hadi wakati huu kila kitu kinapita vizuri. "Mwisho wa kumnukuu.
Katika nchi kavu jeshi la Kenya linasaidiwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Somalia pamoja pia na jeshi la anga. Lakini opereshini hizo zinakorofishwa na hali mbaya ya hewa na njia zisizopitika.
Balozi wa Somalia mjini Nairobi Mohamed Ali Nur anasema:
"Ni jukumu la serikali ya Kenya kujihami na kuilinda nchi na wananchi wake. Wakenya wameingia, hakuna kosa lolote."
Uamuzi wa jeshi la Kenya kujiingiza kusini mwa Somalia umezusha ghadhabu miongoni mwa wanamgambo wa al Shabab walioapa kulipiza kisasi mjini Nairobi ikiwa wanajeshi wa Kenya hawatorudi nyuma.
Serikali ya Kenya imesema hii leo vitisho vya waasi wa Al Shabab haviwashughulishi. "Hatutozuwia, hatuwaogopi Al Shabab" amesema kamanda Chirchir.
Hata hivyo polisi imesema hatua za usalama zimeimarishwa pamoja pia na mfumo wa kukusanya habari na hasa katika jiji la Nairobi.
"Nawatolea mwito raia wote wa Nairobi na Wakenya wote kwa jumla wawe macho kupita kiasi na kuripoti kwa polisi chochote kile watakachohisi ni kigeni au kinatia wasiwasi" amesema mkuu wa polisi wa mkoa wa Nairobi, Antony Kibuchi.
Wakati huo huo, duru za polisi zinasema raia wawili wa Uingereza wanaotuhumiwa kuhusika na harakati za kigaidi wamekamatwa katika mpaka kati ya Kenya na Somalia. Maafisa wa serikali ya Uingereza wamethibitisha habari hizo bila ya kutoa maelezo zaidi.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Afp
Mhariri:Josephat Charo