Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kuendelea na kazi
11 Julai 2005Umoja wa Mataifa umesema vikosi vya kujumuishwa vitaendelea kulinda amani katika mataifa ya mizozo na kusaidia katika maendeleo ya nchi hizo.
Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland ameliambia shirika la habari la IPS kwamba katika ripoti mpya ya Umoja huo imependekezwa vikosi vya kulinda amani na vile vya kuangalia masuala ya kijamii vijumuishwe pamoja katika juhudi za kuleta amani kwenye mataifa hayo.
Ripoti hiyo imegusia kwamba vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vimegeuka kutoka kwenye kulinda amani na kujaribu kuzisaidia nchi hizo kufanya mageuzi ya kuondokana na vita na kuelekea amani pamoja na maendeleo ya muda mrefu.
Kwa mujibu wa ripoti hatua hiyo imewafanya wanajeshi hao kujihusisha katika operesheni mbambali zinazohitaji ujuzi mkubwa pamoja na ushirikiano wa hali ya juu ili kuzifanikisha.
Nchi nyingi za mizozo zimejikuta zimetumbukia kwenye mapigano mengine licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani.
Kwa mujibu wa takwimu uwezekano wa kufeli kwa makubaliano ya amani ni mkubwa zaidi kulikoni wa kupata mafanikio.
Bwana Egeland, mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mshirikishi wa masuala ya misaada ya dharura kwenye Umoja huo amesema ni muhimu kwa kila taifa kufanya juhudi kwa hali na mali ili kujenga jamii zenye amani na maendeleo.
Hata hivyo baadhi ya watu wameelezea wasiwasi wao kwamba uadilifu unaohitajika katika shughuli za kutoa misaada umewekwa hatarini kutokana na kujumuishwa kwa vikosi vya ulindaji usalama na vile vya kutoa misaada katika maeneo ya vita.
Wafanyikazi wa kutoa misaada wanaoshirikiana na Umoja wa Mataifa wanahofia maisha yao kutokana na kuhusishwa na wanajeshi wa Umoja huo.
Wafanyikazi hao wanasema kwamba katika maeneo yaliyo na mizozo kujihusisha na wanajeshi kunaweza kuyahatarisha maisha ya watu na pia kunaifanya kazi yao ya kutoa misaada kuwa ngumu.
Lakini bwana Egeland anashikilia kwamba katika maeneo kunako endelea vita ni lazima kufanyike juhudi zaidi za kuwalinda watoa misaada kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Ameongeza kusema kwamba lazima kuwepo tofauti kati ya wafanyikazi wa kutoa misaada na wanasiasa au wanajeshi.
Huku Ripoti hiyo ikipendekeza ushirikiano wa karibu zaidi kati ya wahusika , baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile shirika la msalaba mwekundu bado linamashaka juu ya kujumuishwa kwa vikosi hivyo.
Msemaji wa shirika hilo amesema ijapokuwa shirika la msalaba mwekundu linaunga mkono ushirikiano wa kuimarisha kazi ya utoaji misaada katika maeneo ya vita,shirika hilo linapinga vikali wazo lolote la ujumuishaji zaidi wa vikosi vya kulinda usalama na vya kutoa misaada.
Shirika hilo huru pia limesema liko tayari kushirikiana na Umoja wa Mataifa lakini haliwezi kufanya kazi yoyote inayoamriwa na Umoja huo. Hata hivyo mshirikishi wa misaada ya kibinadamu wa Umoja huo bwana Egeland ambaye pia alikuwa katibu mkuu wa shirika la msalaba mwekundu la Norway kabla ya kujiunga na Umoja wa Mataifa amesema hatarajii mashirika huru kujijumuisha na Umoja wa Mataifa.
Upande wake Espen Barth Eide kutoka kituo kinachoshughulikia masuala ya kimataifa cha Norway NUPI ambaye pia amehusika katika utayarishaji wa ripoti hiyo,
amesema Umoja wa Mataifa hivi sasa upo katika hali ya mgawanyiko na kwamba hali ni ngumu kwa Umoja huo kuweza kuongoza operesheni mbali mbali zitakazoleta amani ya kudumu na maendelea katika mataifa ya mizozo.