1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya kulinda amani vyashambuliwa Afrika ya Kati

22 Novemba 2016

Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati limesema kuwa moja kati ya vituo vyake vilishambuliwa kwa risasi wakati yalipozuka mapambano kati ya makundi mawili yanayohasimiana.

Zentralafrikanische Republik Bangui MINUSCA UN Truppen
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Matumizi hayo ya nguvu yameibuka jana jumatatu baina ya makundi yanayohasimiana ya wale wanaotajwa kuwa ni  waasi wa kundi la Seleka, katika mji wa Bria Kilometa 400 kaskazini mashariki mwa Bangui vimesema vikosi hivo katika taarifa yake.

Vituo vya jeshi hilo la kulinda amani la Umoja wa Mataifa vililengwa na chama cha wananchi kwa ajili ya mwamko katika Jamhuri ya Afrika ya kati FPRC kabla ya kuondolewa katika eneo hilo kufuatia mapambano ya risasi  ya kulipiza kisasi.

Chama cha wananchi kwa ajili ya mwamko wa Jamhuri ya Afrika ya kati  FPRC ni kundi lililojitenga, liliongozwa na Noureddine Adam ambaye anakabiliwa na vikwazo kutokana na madai ya kushiriki katika mauaji ya mwaka 2013 na 2014.

Kundi jingine la waasi wa zamani wa Seleka  lililohusika katika mapigano hayo siku ya jumatatu ni lile la the Union for Peace in Cetral Afrika UPC ambalo linaongozwa na  Ali Ndarass.

Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema kuwa makundi hayo mawili yanaweza kuhusishwa na kuwajibishwa kutokana na machafuko hayo hasa madhara ambayo yamewalenga raia, wakati hayo yakiwa yanaendelea shirika la umoja wa mataifa linalohudumia watoto UNICEF limesema kuwa mmoja kati ya watoto watano nchini humo hawana makazi  kufuatia machafuko ambayo yaliua maelfu ya watu.

Watoto nchini humo wako katika hatari kwa kukosa makaazi

Shirika hilo limesema kuwa zaidi ya watu 850,000 nusu yao wakiwa watoto nchini humo wameyakimbia makazi yao na wengine wamekimbila katika nchi jirani za Cameroon, Chad, Congo na Congo Brazavile kwa ajili ya kutafuta hifadhi.

Baadhi ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wakitafuta hifadhi Hangar.Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Belluz

Mwakilishi mkuu wa siasa nje ya Umoja wa Ulaya  Federica Mogherini amesema kuwa Mpango wa makubaliano kati ya wafadhili na jamhuri ya afrika ya kati ni mkubwa na kabambe,na kuitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ili kufikiwa kwa utekelezaji wa mpango huu.

Jamhuri ya Afrika ya kati moja kati ya nchi masikini zaidi duniani ambayo imekuwa ikijitahidi kurejea katika hali ya kawaida baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliibuka mwaka 2013 kufuatilia kupinduliwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Francois Bozize ambaye alikuwa mkisto na kisha kuondolewa na kundi la waaasi wa kiislam kutoka muungano wa Seleka.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu