1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Marekani kuondoka rasmi Iraq

Bruce Amani15 Desemba 2011

Majeshi ya Marekani yameshusha bendera yao nchini Iraq leo katika sherehe rasmi, kabla ya kuondoka kwao nchini humo miaka tisa baada ya uvamizi wenye utata uliofanywa na Marekani kumwondoa madarakani Saddam Hussein.

Rais Barack Obama akiwasalimu wanajeshi wa Marekani kwenye kambi ya Fort Bragg.
Rais Barack Obama akiwasalimu wanajeshi wa Marekani kwenye kambi ya Fort Bragg.Picha: dapd

Hafla ya kuashiria kufungwa kwa makao makuu ya jeshi la Marekani nchini Iraq inajiri siku moja tu baada ya rais wa Marekani Barack Obama kusifu ufanisi mkubwa wa kivita kwenye hotuba yake aliyotoa hapo jana ya kuwakaribisha nyumbani baadhi ya wanajeshi wake.

Kuna takriban wanajeshi 4,000 wa Marekani nchini Iraq, lakini wataondoka nchini humo katika siku sijazo, hadi wakati ambao hakutakuwa tena na wanajeshi wa Marekani watakaosalia nchini humo ambako kulikuwa na zaidi ya wanajeshi 170,000 katika zaidi ya kambi za kijeshi 500.

Kujiondoa huko kutamaliza vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya Wairaqi na karibu wanajeshi 4,500 wa Marekani, wengine wengi kujeruhiwa, na zaidi ya raia milioni moja mia tano wa Iraq kuwachwa bila makao.

Katika kituo cha ndege cha Fort Bragg jimbo la North Carolina, rais Obama alishangiliwa na wanajeshi huku akiadhimisha takriban miaka tisa ya uvujaji damu na ujenzi wa Iraq.

Nchini Afghanistan, waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta alisema ataelekea nchini Iraq kuhudhuria sherehe hiyo ya kuishusha bendera na kuashiria kumalizika kwa vita ambavyo wamevifanya kama nchi.

Rais Obama akiwahutubia wanajeshi kwenye kambi ya Fort Bragg.Picha: dapd

Obama aliongeza kusema kuwa hii leo mojawapo ya kurasa muhimu za historia ya jeshi la Marekani zitafungwa. Mustakabali wa Iraq utakuwa mikononi mwa watu wake. Vita vya Marekani vitakwisha. Alisema Obama. Aliwaambia wanajeshi kuwa jukumu lao lilikuwa kuiunda Iraq ambayo ingekuwa huru na kujitegemea, ambayo ingeweza kujiongoza na kujilinda yenyewe.

Mtangulizi wa Obama George W Bush aliamuru uvamizi nchini Iraq mnamo mwaka 2003, akisema kuwa kiongozi wa wakati huo Saddam Hussein alikuwa akiuhatarisha ulimwengu na mipango yake ya kuunda silaha za uharibifu mkubwa. Saddam aling'olewa madarakani na kisha kunyongwa lakini hakuna silaha zozote za aina hiyo zilizopatikana.

Obama aliiunda taaluma yake ya kisiasa kwa kupunga vita hivyo. Mnamo mwaka 2002, alivipinga vita vya aina hiyo kama vile vya Iraq na akatumia mbinu hiyo kuingia ikulu ya White House kwa kuahidi kuwarejesha nyumbani wanajeshiwa Marekani walioko vitani.

Iraq sasa ina bunge na uchaguzi wa kawaida, na itaongozwa na serikali ya Kishia ambayo ilichukua mahali pa utawala uliojaa Wasunni wake Saddam Hussein.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Abdulrahman