1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Msumbuji, Rwanda vyakomboa mji muhimu

9 Agosti 2021

Vikosi vya Msumbiji vikisaidiwa na wanajeshi wa Rwanda vimewafurusha wanamgambo wa itikadi kali waliokuwa wanaudhibiti mji muhimu wa bandari wa Mocimboa da Praia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo lenye utajiri wa gesi

Kigali, Ruanda | Soldaten aus Ruanda auf dem Weg nach Mozambique
Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Msemaji wa Wizara ya ulinzi ya Msumbiji Kanali Omar Saranga alisema katika kikao cha waandishi wa habari mjini Maputo kuwa sasa wanayadhibiti majengo ya serikali, bandari, uwanja wa ndege, hospitali na vituo vingine muhimu. Mji wa Mocimboa da Praia ambako mashambulizi ya kwanza ya itikadi kali yalifanywa Oktoba 2017, tangu mwaka jana umetumika kama makao makuu ya wapiganaji wenye mahusiano na Kundi linalojiita Dola la Kiislamu - IS, wakijiita Al-Shabaab nchini humo.

Msemaji wa jeshi la pamoja Kanali Ronald Rwivanga amesema mji huo wa bandari ulikuwa ngome ya mwisho ya wanamgambo hao na kukombolewa kwake kunaashiria mwisho wa awamu ya kwanza ya operesheni za kupambana na uasi wa itikadi kali.

Wanajeshi wa Msumbuji wamekuwa wakipambana kukamata udhibiti wa mkoa wa Cabo Delgado, eneo lenye mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya gesi asilia – mradi wa dola bilioni 20 unaoendeshwa na kampuni kubwa ya nishati ya Total ya Ufaransa.

Kampuni ya Total ilifunga shughuli zake Cabo DelgadoPicha: DW

Rwanda ilipeleka askari 1,000 mwezi uliopita ili kulipiga jeki jeshi la Msumbuji. Wiki iliyopita walipata mafanikio yao ya kwanza tangu walipoingia nchini humo, wakisema wamelisaidia jeshi la Msumbuji kukamata udhibiti wa Awasse – eneo dogo lakini pia la kimkakati la makazi karibu na Mocimboa da Praia

Soma zaidi:Afrika ya Kusini kupeleka wanajeshi 1,500 nchini Msumbiji

Shirikia linalofuatilia mgogoro huo la ACLED limesema karibu watu 800,000 walikimbia makazi yao huku 3,100 wakiuawa – nusu yao wakiwa ni raia.

Kanali Rwivanga amesema wataendelea na operesheni za usalama ili kuyasafisha kabisa maeneo hayo na kuwaruhusu wanajeshi wa Msumbuji na Rwanda kufanya operesheni za kurejesha utulivu, na kuwawezesha watu kurejea makwao na kufunguliwa kwa biashara.

Baada ya awali kukataa msaada wa kigeni, wanajeshi wa Rwanda walipelekwa nchini humo Julai 9 kufuatia ziara ya Aprili ya kiongozi wa Msumbuji Filipe Nyusi.

Soma zaidi: WFP yaomba dola milioni 121 kuwasaidia watu wa Cabo Delgado

Wiki chache baadaye wakafwatwa na wanaejshi kutoka nchi jirani za Afrika Kusini, Zimbabwe na Angola ambazo zinapeleka askari wao chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC.

Shirika la Save The Children limesema leo kuwa idadi kubwa ya watoto wanaokimbia machafuko yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo. Ripoti ya shirika hilo imesema kwa mwezi mmoja uliopita, idadi ya Watoto wasioandamana na watu wanaokimbia mapigano katika mkoa wa Cabo Delgado imepanda kwa asilimia 40. Mpaka sasa jumla ya wasichana na wavulana 336,000 wamekimbia.

AFP/DPA