1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Vikosi vya RSF nchini Sudan vimefanikiwa kuingia Wad Madani

19 Desemba 2023

Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM limesema watu wapatao 300,000 wamelikimbia jimbo la El Gezira nchini Sudan tangu Disemba 15 kufuatia mapigano kati ya wanamgambo wa RSF na jeshi la nchi hiyo.

Sudan | Wanamgambo wa RSF
Wanamgambo wa RSF wakiwa mji mkuu wa Sudan KhartoumPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Vikosi vya RSF ambavyo vinapambana na jeshi la Sudan kwa muda wa miezi minane sasa, vimekuwa vikiukaribia mji mkuu wa jimbo hilo Wad Madani.

Mashuhuda wameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wapiganaji wa RSF wamefanikiwa kuingia Wad Madani jana Jumatatu.

Wameongeza kuwa RSF imechukua udhibiti wa makao makuu ya jeshi, kituo cha polisi na hospitali baada ya mapigano yaliyodumu kwa saa moja katika mji huo.

Vidio zilizochapishwa na RSF zimeonyesha wapiganaji wake wakiwa kwenye magari ya kubebea mizigo kwenye mitaa ya Wad Madani na kwenye daraja upande wa Blue Nile, sehemu walizokuwa wakipigana na jeshi.

Iwapo RSF itafanikiwa kuchukua udhibiti kamili wa Wad Madani, mji uliojaa watu waliokimbia maakazi yao na ndio kitovu cha misaada, huenda ikawafungulia njia kuingia pia katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Sudan.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW